ISTANBUL-Mjumbe wa ujumbe wa Bunge la Tanzania, Dkt.Zeyana Abdallah Hamid, ameshiriki kongamano la mtandao wa wabunge wa ngazi ya juu lililojikita katika kuimarisha afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana wakati wa majanga na migogoro.
Kongamano hilo liliandaliwa na Mtandao wa Mabunge unaosimamiwa na Global Leaders Network for Women’s, Children’s and Adolescents’ Health na lilifanyika Aprili 17, 2026 katika Hoteli ya Radisson Blu Sisli jijini Istanbul, Uturuki, pembeni ya Mkutano wa 152 wa Bunge la Dunia (IPU).
Mkutano huo ulijadili namna ya kuharakisha hatua za mabunge katika kukuza matumaini, amani na kuhakikisha afya na ustawi wa wanawake, watoto na vijana unaendelea kulindwa wakati wa majanga na migogoro ya kibinadamu.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt Zeyana alisema wabunge wana wajibu wa kuhakikisha huduma muhimu za afya zinaendelea kutolewa bila kukatizwa hata wakati wa dharura au migogoro.
Alieleza kuwa huduma kama afya ya uzazi kwa mama, programu za lishe, chanjo pamoja na huduma za kinga kwa wanawake, watoto na vijana zinapaswa kupatikana wakati wote.
“Bunge lina nafasi muhimu kuhakikisha kuwa wakati wa dharura na migogoro, huduma za afya ya uzazi, lishe, chanjo na huduma za kinga kwa wanawake, watoto na vijana haziathiriki,” alisema.
Kwa mujibu wake, hilo linaweza kufikiwa kupitia kutungwa kwa sheria zinazounga mkono huduma hizo, kupitisha bajeti za kutosha na kuimarisha ufuatiliaji ili kuhakikisha utekelezaji mzuri wa programu za afya.
Dkt Zeyana pia alisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuweka afya ya mama na mtoto kuwa ajenda muhimu ya taifa.
“Msisitizo wa Tanzania ni kwamba hakuna mtu anayepaswa kuachwa nyuma. Afya ya uzazi ni haki, si upendeleo,” alisema akiongeza kuwa ataendelea kuutetea ajenda hiyo ndani ya Bunge.
Wakati huo huo, makatibu wa mabunge kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) walikutana pia jijini Istanbul kubadilishana uzoefu na mikakati ya kuimarisha utendaji wa mabunge.
Mkutano huo, ambao pia ulifanyika pembezoni mwa Mkutano wa 152 wa IPU, ulijadili nafasi ya makatibu wa mabunge katika kuharakisha utekelezaji wa maazimio ya IPU, kuongeza uwazi na kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za mabunge.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni ubunifu wa kidijitali katika mabunge, ufanisi wa kiutawala pamoja na ushirikiano wa kikanda.
Tanzania iliwakilishwa katika kikao hicho na Daniel Eliufoo aliyeshiriki kwa niaba ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika majadiliano hayo, alieleza hatua ambazo Tanzania imepiga katika kuboresha mifumo ya Bunge, ikiwemo kuanzishwa kwa jukwaa la Bunge Online na mfumo wa E-Parliament ikiwa ni sehemu ya juhudi za kisasa za kuimarisha michakato ya utungaji sheria kulingana na ajenda ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya Bunge kupitia mageuzi ya kidijitali ikiwemo jukwaa la Bunge Online na mfumo wa E-Parliament, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ufanisi, uwazi na uwajibikaji katika kazi za Bunge,” alisema Bw Eliufoo.

