ISTANBUL-Makatibu wa Mabunge kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) wamekutana leo Istanbul, Uturuki, kubadilishana uzoefu na mikakati ya kuimarisha utendaji wa mabunge.
Mkutano huo umefanyika pembezoni ya Mkutano wa 152 wa IPU, ukilenga kuangazia nafasi ya Makatibu wa Mabunge katika kuharakisha utekelezaji wa maazimio ya IPU, kuboresha uwazi, na kuimarisha usimamizi wa shughuli za kibunge.
Mada zilizojadiliwa katika kikao hicho ni Ubunifu wa Kidijitali Bungeni, Ufanisi wa Kiutawala na Ushirikiano wa Kikanda.Tanzania imeshiriki kikao hicho kupitia Mwakilishi wa Katibu wa Bunge Ndg. Daniel Eliufoo ambaye alieleza hatua zilizopigwa katika kuboresha mifumo ya kibunge, ikiwemo Bunge Mtandao na mfumo wa E-Parliament kuelekea Dira 2050.



