TEF yalaani uvamizi katika ofisi za Gazeti la Pambazuko,yataka hatua za haraka zichukuliwe

NA DIRAMAKINI

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limelaani vikali tukio la uvamizi katika ofisi za Gazeti la Pambazuko zilizopo Kijitonyama, jijini Dar es Salaam, ambapo watu wasiojulikana walivamia na kuiba baadhi ya vifaa pamoja na nyaraka muhimu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 11,2026 na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Aprili 10, 2026, na limeelezwa kuwa ni la kusikitisha na lenye kuashiria hatari kwa usalama wa vyombo vya habari nchini.

TEF imezitaka mamlaka husika, hususan vyombo vya dola, kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika wa tukio hilo na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kisheria bila kuchelewa.

Jukwaa hilo limesisitiza kuwa kulinda usalama wa wanahabari na taasisi za habari ni wajibu wa msingi wa dola na jamii kwa ujumla.

Aidha, TEF imeeleza kuwa matukio ya aina hiyo yanahatarisha uhuru wa vyombo vya habari na yanaweza kudhoofisha juhudi za wanahabari katika kutekeleza majukumu yao ya kuwahabarisha wananchi.

Katika hatua nyingine, Jukwaa hilo limetoa pole kwa uongozi na wafanyakazi wa Gazeti la Pambazuko kufuatia tukio hilo, na kuahidi kusimama nao katika kuhakikisha mazingira salama ya utendaji wa kazi za uandishi wa habari yanaendelea kudumishwa nchini.

“Tunatoa wito kwa mamlaka na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kulinda usalama wa wanahabari na vyumba vya habari, ili kuhakikisha uhuru wa habari unalindwa na kuheshimiwa wakati wote. Mungu ibariki Tanzania,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here