DODOMA-Mamlaka ya Uteuzi imeridhia maombi ya muda wa ziada kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 hivyo imeiongezea tena muda wa siku ishirini na moja (21) na kuitaka ikamilishe kazi kabla au ifikapo Aprili 24, 2026.
Mamlaka hiyo imeeleza sababu za kuongeza muda huo kwa Tume ni pamoja na kuiwezesha Tume kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa na maoni yaliyopokelewa, kutoa fursa kwa wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi kufanyia kazi baadhi ya vielelezo vipya vilivyowasilishwa.
Sababu nyingine ni kuiwezesha Tume kukamilisha maandalizi ya Ripoti itakayowasilishwa kwa Rais na kutoa fursa kwa Tume kuandaa tafsiri ya Ripoti hiyo.
Tume hiyo ilianza kutekeleza majukumu yake Novemba 20, 2025 na kutarajiwa kukamilisha kazi yake ndani ya kipindi cha siku 90.
Hata hivyo, kutokana na sababu mbalimbali, Tume iliongezewa muda wa kukamilisha kazi na kutakiwa kuwasilisha Ripoti kwa Rais kabla au ifikapo April 3, 2026.
Hivyo, kufuatia nyongeza ya muda, wananchi waliendelea kujitokeza kwa wingi tofauti na matarajio ya Tume. Hivyo, Tume iliendelea kupokea ushahidi, taarifa na maoni zaidi. Kwa sababu hiyo, Tume haikuweza kukamilisha kazi yake ndani ya muda wa nyongeza uliotolewa na hivyo kulazimika kuomba muda wa ziada ili kukamilisha kazi yake.
Tume inaendelea kuwashukuru wananchi na wadau wote waliotoa ushirikiano kwa Tume wakati wa kufanya uchunguzi, ikiwemo wale waliofika mbele ya Tume kutoa ushahidi, taarifa na maoni, waliopiga simu na kutuma ujumbe, waliotuma ushahidi, taarifa na maoni kwa maandishi na waliowasiliana na Tume kwa njia za mitandao ya kijamii.

