DODOMA-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuboresha bajeti ya elimu wakati ikitekeleza mtaala mpya wa elimu ili kuziba mianya ya mahitaji shuleni.
“Kwa kuwa tunaenda katika mtaala mpya wa elimu, tutaendelea kuboresha bajeti. Tutaendelea kuboresha bajeti kwa sababu mahitaji yanaongezeka kila wakati katika kumfanya mtoto asome vizuri,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Aprili 9, 2026 wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Agnesta Lambert Kaiza, kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali juu ya kukomesha michango holela inayotozwa shuleni.
Dkt. Mwigulu amesema Serikali haina shida na michango ya chakula ambayo imekuwa ikitolewa shuleni lakini akasisitiza kuwa endapo kutatokea michango mingine yoyote, ni lazima ifuate miongozo ya serikali na ipate baraka za Wakuu wa Mikoa husika.
Akitoa mfano wa michango ambayo haikubaliki, Waziri Mkuu amesema akiwa ziarani mkoani Katavi, alipokea malalamiko ya Mama mmoja ambaye mwanaye alizuiwa kujiunga na shule ya sekondari hadi atoe sh. 50,000/- ya dawati.
“Nilielekeza yule mtoto arudishwe shuleni na nimpongeze Mkuu wa Mkoa ambaye amenijulisha kuwa yule mtoto amesharudi shuleni. Lakini pia nilielekeza yule mwalimu mkuu naye aitwe na mamlaka za nidhamu, ahojiwe kwa uzembe wa kuona mtoto anakosa masomo kwa miezi miwili na wao wakaendelea na maisha kana kwamba hakuna jambo lililotokea,” amesema.
Mbali na changamoto hiyo, Waziri Mkuu amewapongeza walimu nchini kwa kujitoa bila kuchoka ili kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora.
“Sote tunatambua kuwa walimu wengi wamejitoa sana katika baadhi ya maeneo. Licha ya wingi watoto na uchache wa walimu, kwa juhudi zao wamehakikisha wanakamilisha syllabus zao ili watoto wetu wapate elimu bora.”
Akielezea kuhusu uwepo wa walimu wa kujitolea katika baadhi ya shule, Waziri Mkuu amesema alishatoa maelekezo kwamba malipo ya walimu wa aina hiyo yatoke kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri husika badala ya kuwataka wazazi wachangie malipo yao.
“Wazo la kuwa na walimu wa kujitolea ni jema, na sisi wakati tunasoma tulipata mafunzo ya ziada (tuition) kwa walimu wa aina hii. Wazo la kuwa na walimu wanaojitolea ni jema lakini malipo yao yasilipwe na wazazi, badala ya kwenda kwenye michango, Mamlaka za Serikali za Mitaa watumie mapato ya ndani.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kuimarisha vitengo vya tathmini na ufuatiliaji katika kila wizara ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
“Kwenye kila wizara, kuna hivi vitengo vya ufuatiliaji na tathmini. Tunapanga kuongeza bajeti zao ili viweze kutimiza wajibu wao katika ufuatiliaji wa miradi na shughuli zote za Serikali.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Monduli, Isack Joseph Copriano aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha timu ya tathmini na ufuatiliaji ili kuharakisha majibu ya wananchi na hususan kero zao.
Alisema katika kuimarisha mawasiliano na wananchi, Serikali imeanzisha kituo cha kupokea simu (Call Centre) yenye namba 190 ambapo mwananchi mwenye shida yoyote anaweza kupiga simu na kutoa kero yake na kwamba atajulishwa majibu yake kupitia kituo hicho.
Amesema Serikali inataka kurejesha utaratibu wa kila kiongozi kubeba hoja za wananchi kupitia rejesta ambazo zitakuwa zinatumika kwenye ofisi za viongozi kurekodi kero za wananchi na kutoa mrejesho serikalini kila mwisho wa mwezi.
“Utaratibu wa kupokea kero siyo wa kwenye ziara tu, kila mwezi viongozi watapaswa kutoa taarifa ya idadi ya wananchi waliowahudumia na majibu waliyowapa wakionesha hoja zipi walipokea, namba za simu za wananchi waliohudumiwa na hizo hoja zimetatuliwa vipi.”
“Tunataka kurejesha utaratibu wa kila kiongozi kubeba hoja za wananchi na siyo kuacha wananchi waende kutafuta majibu kwa viongozi,” alisisitiza.
Tags
Bajeti ya Elimu
Bunge la Bajeti
Bunge la Tanzania
Dr Mwigulu Lameck Nchemba
Habari
Ofisi ya Waziri Mkuu



