Uchumi wa Tanzania waendelea kuimarika licha ya changamoto za Kimataifa

NA GODFREY NNKO

WAKATI dunia ikiendelea kukabiliwa na misukosuko ya kiuchumi inayochochewa na mgogoro unaoendelea wa Mashariki ya Kati, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha uimara na mwelekeo chanya, ukiwa na viashiria vinavyoashiria ustahimilivu dhidi ya athari za nje.
Aidha, Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kubakiza Riba ya Benki Kuu (CBR) katika kiwango cha asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka 2026.

Hayo yameelezwa leo Aprili 2,2026 makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) anayeshughulikia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Mwenyekiti wa MPC ambaye pia ni Gavana wa BoT. Bw.Emmanuel Tutuba.

Dkt.Kayandabila amewaeleza wadau wa sekta ya fedha pamoja na waandishi wa habari kuwa, uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichoketi Aprili Mosi, 2026 kwa ajili ya kufanya tathmini ya mwenendo wa uchumi pamoja na mwelekeo wa Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate-CBR).

Katika tathmini yake, Dkt.Kayandabila amesema, kamati ilieleza kuwa ingawa mgogoro wa Mashariki ya Kati unaendelea kuwa tishio kwa uchumi wa dunia, athari zake kwa uchumi wa ndani bado hazijajitokeza kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, kamati imeonya kuwa kuendelea kwa mgogoro huo kwa muda mrefu kunaweza kuathiri matarajio ya ukuaji wa uchumi.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, takwimu zinaonesha kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2026, uchumi ulikua kwa kasi ya asilimia 6.2 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.7 kwa Zanzibar. Dkt.Kayandabila amesema, ukuaji huu umechangiwa zaidi na sekta za ujenzi, kilimo, huduma za fedha, bima pamoja na utalii.

Amesema, mwenendo huo umeenda sambamba na kuimarika kwa mikopo kwa sekta binafsi, ambayo imekua kwa wastani wa asilimia 22.8, ikichochewa na ongezeko la mahitaji ya mikopo kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

Kwa mujibu wa MPC, katika robo ya pili ya mwaka 2026, uchumi unatarajiwa kuendelea kukua kwa asilimia 6.1 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.6 kwa Zanzibar, endapo hakutakuwa na mshtuko mkubwa wa kiuchumi kutoka nje.

Kuhusu mfumuko wa bei, Dkt.Kayandabila amesema, kamati ilibaini kuwa umeendelea kudhibitiwa ndani ya lengo la sera ya fedha, ambapo ulikuwa wastani wa asilimia 3.3 kwa Tanzania Bara na asilimia 4.5 kwa Zanzibar katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.

Dkt.Kayandabila amesema, mafanikio haya yamechangiwa na utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha pamoja na utulivu wa bei za chakula na nishati.

Aidha,MPC imeeleza kuwa, athari za awali za kupanda kwa bei za nishati na gharama za usafirishaji bado hazijajitokeza kikamilifu katika viwango vya mfumuko wa bei.

Hata hivyo, matarajio ni kuwa mfumuko wa bei utaendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5 katika robo ya pili ya mwaka 2026, ukisaidiwa na uthabiti wa thamani ya shilingi na utulivu wa bei za chakula.

Sekta ya benki imeendelea kuwa imara, ikiwa na ukwasi wa kutosha pamoja na viwango vya mtaji vinavyoweza kukabiliana na vihatarishi mbalimbali.

Dkt.Kayandabila amesema,ubora wa mikopo umeimarika zaidi, ambapo uwiano wa mikopo chechefu umeshuka hadi asilimia 2.9, chini ya kiwango cha juu kinachokubalika cha asilimia tano.Sambamba na hilo, mifumo ya malipo imeendelea kufanya kazi kwa ufanisi.

Amesema, katika sekta ya nje, urari wa malipo ya kawaida umeendelea kuimarika, ukikadiriwa kufikia nakisi ya asilimia 2.2 ya Pato la Taifa kwa mwaka unaoishia Machi 2026, ikilinganishwa na asilimia 2.4 mwaka 2025.

Naibu Gavana huyo amesema, mafanikio haya yametokana na ongezeko la mauzo ya nje, hususan dhahabu, mazao ya kilimo na huduma za utalii.

Kwa upande wa Zanzibar, amesema urari huo umeendelea kuwa na ziada kutokana na mapato ya utalii.

Vilevile, thamani ya shilingi imeendelea kuimarika dhidi ya fedha za kigeni, ikisaidiwa na uwepo wa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni inayozidi dola za Marekani bilioni 6.2, kiasi kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.8.

Dkt.Kayandabila amesema, kiwango hiki kinazidi vigezo vya chini vya kitaifa na kikanda.

Kwa upande wa utekelezaji wa sera ya bajeti, kamati imeeleza kuridhishwa na mwenendo wake, ambapo makusanyo ya kodi yamevuka malengo yaliyowekwa, yakichangiwa na ukuaji wa uchumi, ufanisi katika usimamizi wa kodi, pamoja na kuongezeka kwa ulipaji wa kodi kwa hiari.

Pia, Dkt.Kayandabila amesema,matumizi ya Serikali nayo yameendelea kufanyika kwa kuzingatia rasilimali zilizopo.

Kutokana na mwenendo huo,MPC imeihimiza Benki Kuu kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya mgogoro wa Mashariki ya Kati na athari zake kwa uchumi wa taifa, ili kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za sera kwa wakati muafaka.

Dkt.Kayandabila amesema kuwa, kikao kijacho cha Kamati ya Sera ya Fedha kinatarajiwa kufanyika mwezi Julai,mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here