NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa, Tanzania inaendelea kuimarisha nafasi yake katika kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI), hali inayoakisi kuimarika kwa mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Ameyasema hayo Aprili 16,2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027.Profesa Mkumbo ameeleza kuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Uwekezaji Duniani ya mwaka 2025 iliyotolewa na Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), mtiririko wa uwekezaji nchini umeongezeka kwa kasi, ukifikia dola za Marekani bilioni 1.72 mwaka 2024 kutoka dola bilioni 1.34 mwaka 2023, sawa na ukuaji wa asilimia 28.3.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Tanzania ilishika nafasi ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji kutoka nje, nyuma ya Ethiopia na Uganda, huku ikiizidi Kenya na Rwanda.
Hata hivyo, pamoja na kushika nafasi hiyo, Tanzania imeongoza kwa kasi ya ukuaji wa uwekezaji katika ukanda huo, ikiwa juu ya wastani wa asilimia 12 wa kanda.
Aidha, katika ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania imeendelea kushika nafasi ya kati kuelekea juu, ikikadiriwa kuwa kati ya nafasi ya tano na sita, nyuma ya nchi zinazoongoza kama Afrika Kusini, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambazo zinanufaika zaidi na uwekezaji mkubwa katika sekta za mafuta, gesi na madini.
Kwa ujumla, Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 11 bora barani Afrika kwa ukubwa wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje.
Profesa Mkumbo amefafanua kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kiwango cha uwekezaji kutoka nje nchini kimeongezeka kutoka dola milioni 944 mwaka 2020 hadi dola bilioni 1.72 mwaka 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 45.1.
Amesema,sekta zilizoongoza kuvutia uwekezaji huo ni madini, uzalishaji viwandani, huduma za fedha na bima, pamoja na habari na mawasiliano, ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 82.4 ya uwekezaji wote mwaka 2023.
Pia, amebainisha kuwa nchi kumi zilizoongoza kuwekeza nchini ni pamoja na Visiwa vya Cayman, Mauritius, Uingereza, Uholanzi, China, Canada, Afrika Kusini, Barbados, Kenya na Nigeria.
Kwa upande wa usajili wa miradi ya uwekezaji, Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesajili jumla ya miradi mipya 611 yenye thamani ya dola za Marekani milioni 6,233.97 hadi kufikia Machi 2026, ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira mpya 102,463.
Vilevile, miradi 45 ya upanuzi yenye thamani ya dola milioni 586.12 imesajiliwa, ikitarajiwa kutoa ajira 9,472.
Waziri huyo amesema, sekta zilizoongoza kwa usajili wa miradi hiyo ni uzalishaji viwandani, usafirishaji, ujenzi wa majengo ya biashara, utalii na kilimo. Kijiografia, mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Arusha, Mwanza na Dodoma imeongoza kwa kuvutia uwekezaji.
Katika maeneo maalumu ya kiuchumi (SEZ), miradi 19 yenye thamani ya dola milioni 331.51 imesajiliwa, ikitarajiwa kuzalisha ajira 11,762 na mauzo ya nje yenye thamani ya dola milioni 885.23.
Miradi hiyo inatekelezwa katika mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Lindi, Njombe, Ruvuma, Kilimanjaro, Pwani, Mtwara, Arusha, Dodoma, Tanga na Dar es Salaam.
Kwa mwaka 2025 pekee, TISEZA ilisajili miradi 915 yenye thamani ya dola bilioni 10.95, ikiwa ni rekodi ya juu zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa usajili wa miradi ya uwekezaji mwaka 1996.
Profesa Mkumbo amesema, katika kipindi cha miaka mitano, idadi ya miradi imeongezeka kutoka 256 mwaka 2021 hadi 915 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 257.4.
Amebainisha kuwa,Serikali imeanza kukusanya takwimu za uwekezaji unaofanywa na kampuni za Kitanzania nje ya nchi, ambapo hadi sasa zaidi ya dola bilioni 3.1 zimewekezwa katika mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Zambia, Afrika Kusini, Japan na Qatar.
Uwekezaji huo unalenga kuongeza ushindani wa kampuni za ndani, kupanua masoko ya bidhaa na kukuza uhamishaji wa teknolojia.
Amesema, ukuaji huo wa uwekezaji ni matokeo ya juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara, akiwapongeza viongozi wakuu wa nchi kwa mchango wao, hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Wakati huo huo,Profesa Mkumbo amewasilisha bungeni ombi la kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 144.85 kwa ajili ya Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 126.01 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 18.83 kwa miradi ya maendeleo.
Aidha,kwa mujibu wa mgawanyo wa mafungu, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji imetengewa shilingi bilioni 35.38, Tume ya Taifa ya Mipango shilingi bilioni 48.64, huku Ofisi ya Msajili wa Hazina ikitengewa shilingi bilioni 60.82.
Profesa Mkumbo amesisitiza kuwa, bajeti hiyo imelenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo, kuboresha usimamizi wa rasilimali za umma, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji na mipango thabiti ya maendeleo ya muda mrefu.
Tags
Bunge la Bajeti
Bunge la Tanzania
Habari
Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji
Prof. Kitila Alexander Mkumbo
Uwekezaji Tanzania