MWANZA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imeendesha programu ya elimu ya fedha kwa wachimbaji wadogo wa madini iliyofanyika tarehe 14 hadi 20 Aprili 2026 katika mikoa ya Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Simiyu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha kiuchumi na kuwaingiza katika mfumo rasmi wa fedha.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea wachimbaji uelewa kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, umuhimu wa kuweka akiba, matumizi ya huduma rasmi za kifedha, pamoja na fursa za kupata mikopo kupitia taasisi za fedha.
Aidha, washiriki walipatiwa elimu juu ya uwekezaji katika dhamana za Serikali, matumizi ya mifumo ya malipo ya kidigitali, na taratibu za kushughulikia malalamiko ya huduma za fedha.Katika programu hiyo, BoT pia ilieleza kuhusu mifuko ya udhamini wa mikopo inayosaidia wajasiriamali, ikiwemo wachimbaji wadogo na wa kati, kupata mitaji kwa urahisi hata wanapokosa dhamana ya kutosha. Mifuko hiyo inachochea upatikanaji wa mikopo na kukuza uzalishaji, hususan katika sekta ya madini.
Kwa upande wa teknolojia, wachimbaji walihamasishwa kutumia mifumo rasmi ya malipo ya kidigitali ili kuongeza usalama, uwazi na ufanisi katika biashara zao. Ilielezwa kuwa, matumizi ya mifumo hiyo husaidia kupunguza gharama, kurahisisha miamala, na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa haraka.

