EWURA yatangaza bei ya mafuta kwa Aprili,2026

NA DIRAMAKINI

BEI za bidhaa za mafuta ya petroli nchini zimeongezeka kwa kiwango kikubwa katika mwezi Aprili 2026 ikilinganishwa na mwezi uliotangulia, hali inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na mwenendo usiotabirika wa soko la kimataifa, uliotikiswa na mivutano ya kisiasa na kiusalama katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo Aprili 1,2026 na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ongezeko hilo linahusisha bidhaa zote kuu za mafuta, ikiwemo petroli, dizeli na mafuta ya taa, zinazoingizwa nchini kupitia bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.

Bei hizo zimepangwa kwa kuzingatia gharama halisi za uagizaji pamoja na mabadiliko ya bei katika soko la dunia.

Kwa mwezi Aprili 2026, bei kikomo za rejareja kwa lita jijini Dar es Salaam zimefikia shilingi 3,820 kwa petroli, shilingi 3,806 kwa dizeli na shilingi 3,684 kwa mafuta ya taa.

Katika Jiji la Tanga, petroli inauzwa kwa shilingi 3,881, dizeli shilingi 3,867 na mafuta ya taa shilingi 3,745.

Aidha, kwa upande wa Mtwara, petroli ni shilingi 3,912, dizeli shilingi 3,898 huku mafuta ya taa yakifikia shilingi 3,777 kwa lita.

Takwimu hizi zinaonesha ongezeko kubwa ukilinganisha na bei za mwezi Machi 2026, ambapo katika Jiji la Dar es Salaam petroli iliuzwa kwa shilingi 2,864 kwa lita, dizeli shilingi 2,858 na mafuta ya taa shilingi 2,932.

Hali kama hiyo ilijitokeza pia katika miji ya Tanga na Mtwara, ambako bei zilikuwa chini kwa viwango vinavyokaribiana na hivyo vya Dar es Salaam.

Kwa upande wa bei za jumla, Aprili 2026 imeonesha pia kupanda kwa gharama. Jijini Dar es Salaam, petroli inauzwa kwa shilingi 3,677.71 kwa lita, dizeli shilingi 3,663.29 na mafuta ya taa shilingi 3,542.70.

Katika Tanga, petroli ni shilingi 3,685.00 na dizeli shilingi 3,659.28, huku Mtwara petroli ikiwa shilingi 3,669.32 na dizeli shilingi 3,669.98 kwa lita.

Ongezeko hili linatajwa kuwa kubwa zaidi ukilinganisha na Machi 2026, ambapo bei za jumla katika Dar es Salaam zilikuwa shilingi 2,723.97 kwa petroli, shilingi 2,718.21 kwa dizeli na shilingi 2,792.70 kwa mafuta ya taa.

Mabadiliko kama hayo yalishuhudiwa pia katika mikoa ya Tanga na Mtwara.

Chanzo kikuu cha kupanda kwa bei hizo kinahusishwa na kuendelea kwa mgogoro wa kijeshi kati ya Marekani kwa kushirikiana na Israel dhidi ya Iran ulioanza Februari 28, 2026.

Mgogoro huo umeathiri kwa kiasi kikubwa miundombinu ya uzalishaji na usambazaji wa mafuta duniani, ikiwemo mashambulizi dhidi ya visima vya mafuta, maghala ya kuhifadhi na viwanda vya kusafisha mafuta.

Aidha, kufungwa kwa Lango la Hormuz-njia muhimu inayopitisha takribani asilimia 20 ya mafuta yote duniani-kumezidisha changamoto ya upatikanaji wa nishati hiyo.

Hali hiyo imesababisha kupungua kwa uzalishaji katika nchi za Mashariki ya Kati na kuongeza gharama za usafirishaji pamoja na bima ya meli za mafuta.

Kutokana na hali hiyo, ongezeko la bei za mafuta limekuwa ni changamoto ya kimataifa. Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unabaki kuwa wa uhakika na kwa bei inayoweza kumuduwa na wananchi, huku athari za kiuchumi na kijamii zikidhibitiwa kadri inavyowezekana.

Wananchi wametakiwa kutumia nishati hiyo kwa uangalifu na ufanisi zaidi katika kipindi hiki cha mabadiliko ya soko.

Pia, wametakiwa kufuatilia taarifa za bei kikomo kupitia simu za mkononi kwa kupiga 15200# na kufuata maelekezo, huduma ambayo ni bure katika mitandao yote ya simu nchini.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015 (Kifungu cha 166), bei za mafuta zinaendelea kuamuliwa na nguvu za soko, huku EWURA ikisimamia ushindani wa haki kwa kuweka bei kikomo zinazolenga kulinda maslahi ya watumiaji.

Kampuni za mafuta zinaruhusiwa kuuza bidhaa zao kwa bei za ushindani, mradi hazizidi kiwango cha juu kilichowekwa wala kushuka chini ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa kisheria.

Vituo vya mafuta vinapaswa kuonesha wazi bei za bidhaa zao pamoja na punguzo au vivutio vinavyotolewa, ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi ya ununuzi.

Ni kosa la kisheria kwa kituo cha mafuta kushindwa kuonesha bei wazi, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka taratibu hizo.

Aidha, wauzaji wanapaswa kutoa stakabadhi za mauzo kupitia mashine za kielektroniki (EFPP), huku wanunuzi wakihimizwa kudai stakabadhi hizo kama uthibitisho wa malipo na ubora wa huduma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here