NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi Mkoa wa Geita limetangaza mafanikio makubwa katika operesheni za kudhibiti uhalifu baada ya kukamata jumla ya watuhumiwa 515 kwa tuhuma mbalimbali katika kipindi cha mwezi Machi 2026.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo hali ya ulinzi na usalama katika mkoa huo imeendelea kuimarika kufuatia juhudi za pamoja kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya usalama pamoja na ushirikiano wa wananchi.
Imeelezwa kuwa katika kipindi hicho, operesheni maalum, misako na doria zilizoendeshwa katika maeneo mbalimbali zimefanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa wanaohusishwa na makosa mbalimbali yakiwemo mauaji, wizi, uvunjaji, kupatikana na mali za wizi, kuingia nchini bila kibali, uzembe, uzururaji, kukiuka masharti ya leseni, kucheza kamari, kujifanya watumishi wa Serikali, pamoja na makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Makosa mengine ni pamoja na kupatikana na nyara za Serikali, uvuvi haramu kwa kutumia nyavu zisizoruhusiwa (timba), utengenezaji wa pombe haramu pamoja na umiliki wa vifaa vya kuchakata madini kinyume cha sheria.
Katika hatua za kisheria zilizochukuliwa, jumla ya kesi 482 zimefunguliwa mahakamani, ambapo kati ya hizo, kesi 261 tayari zimehitimishwa huku watuhumiwa wakipatiwa adhabu mbalimbali kwa mujibu wa sheria. Aidha, kesi 221 zinaendelea kusikilizwa katika hatua tofauti za kisheria.
Katika operesheni hizo, mali na vielelezo mbalimbali vilikamatwa vikiwemo fedha taslimu kiasi cha shilingi milioni 4, pikipiki 15, simu janja 16, simu ndogo 3, ng’ombe 9, mafuta ya dizeli lita 920, jenereta, injini za mitumbwi, pamoja na vifaa vingine kama runinga, spika na sabufa.
Vingine ni pamoja na bangi gramu 700, pembe ya swala, ngozi ya swala, nyavu haramu 166 na pombe haramu lita 459.
Katika jitihada za kuimarisha usalama barabarani, Jeshi la Polisi lilifanya operesheni maalum zilizohusisha magari 6,804 na pikipiki 4,250.
Makosa yaliyobainika ni pamoja na uendeshaji bila leseni, ukosefu wa bima, kutofuata ratiba kwa mabasi, kutovaa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki, kutofunga mikanda ya usalama, pamoja na upakiaji usio salama wa abiria.
Kadhalika, mafanikio katika vyombo vya sheria yameonekana kupitia utolewaji wa hukumu mbalimbali.
Miongoni mwa kesi hizo, baadhi ya watuhumiwa wamehukumiwa vifungo vya muda mrefu gerezani, huku wengine wakitozwa faini kulingana na uzito wa makosa yao.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limeendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa wakati, kushiriki katika vikundi vya ulinzi shirikishi, na kuzingatia sheria za nchi pamoja na tahadhari za usalama, hususan barabarani.
Kwa ujumla, hatua hizi zinadhihirisha dhamira ya dhati ya Jeshi la Polisi ya kuhakikisha amani, utulivu na usalama wa raia na mali zao unaendelea kudumishwa katika Mkoa wa Geita.
Tags
Biashara za Magendo
Genge la Uhalifu
Habari
Jeshi la Polisi Tanzania
Magenge ya Uhalifu
Uhalifu Geita
