Watumishi wa NHIF waiomba Serikali kupitia viwango vya uchangiaji

TANGA-Watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), wameiomba Bodi ya Wakurugenzi kuendelea kuishawishi na kuishauri serikali kufanya mapitio ya viwango vya uchangiaji wa wanachama kupitia kundi la Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi.
Kwa mujibu wa sheria ya Bima ya Afya kwa watumishi wa Umma na wafanyakazi Sekta Binafsi wanachangia asilimia Sita ya mshahara kwa kila mwezi ambapo mwajiriwa anachangia asilimia tatu na mwajiri wake asilimia tatu.

Ombi hili linatokana na ongezeko kubwa la gharama za matibabu kwa sasa pamoja na uwepo wa magonjwa yasiyoambukiza ambayo gharama zake kwenye matibabu ni kubwa.
Akiwasilisha ombi hilo kwa Bodi, Meneja wa NHIF Mkoa wa Tanga Bw. Evance Nyangasi alisema kuwa kutokana na kasi kubwa ya uhitaji wa ubora wa huduma za kibingwa na bingwa bobezi, viwango vya ukuwaji wa technologia na ubunifu wa tiba kwa kuzingatia hali ya uchumi wa dunia katika utaratibu wa ugharamiaji huduma za matibabu umekuwa mkubwa hivyo kusababisha viwango vya sasa vya uchangiaji kushindwa kukidhi mahitaji.

“Kwa sasa gharama za matibabu ni kubwa ikilinganishwa na mwaka 2001 wakati Mfuko ulipoanzishwa, awali huduma zilikuwa ni chache sana lakini kwa sasa kitita cha huduma za matibabu kimeboreshwa na kujumuishwa huduma za kibingwa na bingwa bobezi ambazo gharama zake ni kubwa.

Ili kukabiliana na mabadiliko hayo, aliiomba Bodi kuishauri Serikali ili kupitia viwango hivyo na kuviboresha ili kukidhi mahitaji ya kuboresha zaidi huduma kwa wanachama.
Akijibu hoja za Watumishi Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Bw. Eliud Sanga aliwapongeza kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuwahudumia wanachama na kuimarisha Mfuko.

“Maombi yenu tumeyapokea na sisi Bodi tutaona cha kusaidia ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali katika masuala ya kisera ili Mfuko uendelee kuimarika na kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama,” alisema Bw. Sanga.Bodi imehitimisha ziara yake jana Aprili 15,2026 mkoani Tanga baada ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Mfuko kwa ngazi ya Mkoa katika mikoa ya Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga. Mwenyekiti pia aliambatana na Mjumbe wa Bodi Prof. George Luhago na Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here