NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt.John Mduma amesema kuwa, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) ni miongoni mwa wadau muhimu katika juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyakazi, akisisitiza mchango wake katika kuhamasisha uelewa na utekelezaji wa sheria husika.
WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Sura 263) kwa lengo la kushughulikia masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.Aidha,WCF ambao ni wadhamini wa mkutano huo ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake Julai Mosi,2015 kwa mujibu wa tangazo la Serikali Na.105 la 2011.
Dkt.Mduma ameyasema hayo leo Aprili 16,2026 wakati akifungua mkutano maalum wa wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika Ukumbi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Amesema,ushirikiano kati ya WCF na TEF unalenga kuhakikisha kwamba taarifa sahihi zinawafikia wadau wote, wakiwemo waajiri na waajiriwa ili kuongeza uelewa wa majukumu yao chini ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, waajiri wanapaswa kujisajili katika mfuko huo na kuwasilisha michango kwa wakati, huku waajiriwa wakitakiwa kuhakikisha michango yao inawasilishwa ipasavyo pamoja na kutoa taarifa mapema wanapopatwa na madhila yatokanayo na kazi.
Ameeleza kuwa,utoaji wa taarifa kwa wakati unasaidia mfuko kuchakata madai ya fidia kwa ufanisi, na kwamba fidia hulipwa pale inapothibitika kuwa mfanyakazi amepata madhara ikiwemo ulemavu wa kudumu unaotokana na kazi.
Akizungumzia utendaji wa taasisi hiyo, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa,katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025, WCF ilifanikiwa kuvuka malengo yake kwa kufikia asilimia 104, na kwamba taasisi hiyo imejipanga kuongeza juhudi ili kuvuka zaidi malengo katika kipindi kijacho.
Amebainisha kuwa, kipaumbele kikuu ni kuendelea kutoa elimu kwa waajiri ili wajisajili na kuhakikisha wanaowasilisha michango wanafanya hivyo kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa, ipo haja kwa wanahabari kujiondoa katika hali ya kujizuia au kujitathmini kupita kiasi kabla hata ya kuzuiwa kufanya kazi zao.
Amesema kuwa, hali hiyo imekuwa kikwazo kwa uhuru na ufanisi wa taaluma ya habari.
“Ni wakati sasa wa kuuondoa uoga uliodumu kwa muda mrefu na kurejesha ujasiri katika utekelezaji wa majukumu ya uandishi wa habari,” alisisitiza.
Aidha, Balile ameeleza kuwa, vyombo vya habari vinakabiliwa na changamoto kubwa ya kiuchumi, akibainisha kuwa hali hiyo si ya Tanzania pekee bali ni ya kimataifa.
Amerejea tafiti mbalimbali zinazoonesha kuwa, kati ya mwaka 2005 na 2025, zaidi ya magazeti 3,200 nchini Marekani yalifungwa kutokana na kuyumba kwa uchumi wa sekta hiyo.
Balile ameongeza kuwa, hata nchini Tanzania hali si nzuri, akitolea mfano kampuni ya New Habari ambayo mwaka 2020 ilisimamisha shughuli zake, huku akieleza kuwa vyombo vingine vya habari vikiwemo magazeti, runinga na redio vinaendelea kukabiliwa na changamoto za kifedha.
Kutokana na hali hiyo, Balile amesisitiza umuhimu wa kubuni mikakati mipya ya kiuchumi kwa vyombo vya habari, ikiwemo kutafuta vyanzo mbadala vya mapato vitakavyosaidia kuimarisha uendelevu wa sekta hiyo.
“Tunapaswa kuanza kufikiria upya mwelekeo wa taaluma ya habari na jinsi ya kupata mapato kwa njia bunifu zisizo za kawaida,” ameongeza Balile.
Naye Mjumbe wa Kamati Tendaji ya TEF, Salim Said ameishukuru WCF kwa kuendelea kushirikiana na jukwaa hilo, akisema mchango wa mfuko huo ni muhimu katika kusaidia utekelezaji wa mipango na mikakati ya kukuza na kuendeleza taaluma ya habari nchini.
Mkutano huo wa TEF pia umejadili mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya jukwaa hilo, ambapo wanachama wamepata fursa ya kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha uendeshaji na ufanisi wa taasisi hiyo muhimu katika tasnia ya habari nchini.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF)
TEF Tanzania
WCF Tanzania
