Waziri Makonda asimamisha Uchaguzi wa TOC, avunja uongozi wa sasa

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Paul Christian Makonda umesimamisha uchaguzi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na kuusimamisha uongozi wa sasa wa kamati hiyo kufuatia malalamiko ya baadhi ya wagombea waliokuwa wakiwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TOC kuenguliwa kushiriki katika uchaguzi uliotangazwa kufanyika tarehe 12 Aprili, 2026.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Hassan Mabuye.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,wadau hao wamelalamikia vyombo vilivyosimamia mchakato huo kutokuwa na uwazi,uwajibikaji na kutokutenda haki jambo linalopelekea kukosekana kwa haki za msingi kwa wagombea hao na kuleta taharuki na sintofahamu.

Waziri Makonda amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kuheshimu kikamilifu misingi ya Kimataifa ya uhuru wa Vyama vya Michezo kama inavyoelekezwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (International Olympic Committee).

Aidha, amesema uhuru huo hauondoi wajibu wa kuhakikisha kuwa Taasisi zote zinaendeshwa kwa kuzingatia utawala wa sheria (rule of law), haki, uwazi na uwajibikaji kwa maslahi ya Umma (public interest).

Mheshimiwa Makonda amechukua hatua hiyo kwa mamlaka aliyonayo Kisheria ya kusimamia Sekta ya Michezo Nchini, ikiwemo Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na Sheria za Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 ambazo zinampa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa Sera na kuhakikisha taasisi zote zilizo chini ya Sekta ya Michezo zinaendeshwa kwa kuzingatia sheria, kanuni na misingi ya utawala bora.

Halikadhalika, Waziri Mwenye dhamana ya michezo ana wajibu wa kulinda haki za wanachama wa vyama vya michezo na kuhakikisha usawa na uwazi unazingatiwa wakati wote.

Amesisitiza kuwa, ameshawishika kuchukua hatua hiyo baada ya kuona kuwa mchakato huo uligubikwa na sintofahamu na kutozingatia misingi ya utawala bora kutokana na kuegemea kuwanufaisha watu wachache jambo linazorotesha ustawi wa michezo Nchini.

Pamoja na hatua hizo za muda (temporary and corrective measures), zenye lengo la kupisha uchunguzi huru na kurekebisha kasoro zilizobainika, Mheshimiwa Waziri Makonda atachukua hatua zingine zifuatazo; Kuundwa kwa Uongozi wa muda (Interim Committee) ambapo amewateua wajumbe wafuatao;

1. Ismail Aden Rage - Mwenyekiti

2. Dkt. Steven Mabagala - Makamu Mwenyekiti

3. Amina Mfaume - Katibu

4. Kesi Said Mohammed - Mjumbe

5. Jemedari Said - Mjumbe

6. Asma Hilal - Mjumbe

7. Queen Siraki Mjumbe

Kuundwa kwa Kamati ya Uchunguzi wa kina ambapo ataunda Kamati itakayofanya uchunguzi wa kina kwa kushirikisha vyombo ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Polisi, Vyama vya Michezo na Msimamizi wa Vyama vya Michezo (BMT) kuhusu tuhuma zote zinazohusiana na mwenendo wa Uchaguzi wa TOC kupitia Kamati zote zilizoshiriki kwenye mchakato, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Waziri Makonda amefanya uamuzi hao kwa mujibu wa Kifungu cha
27(2) cha Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Sura ya 49 iliyofanyiwa Marejeo 2023, kinachosema “Kila uamuzi wa Waziri kwa mujibu wa sheria hii uwe wa rufaa au vingine, utakuwa wa mwisho na hutabatilishwa au kubadilishwa na chombo chochote”.

Amefafanua kuwa, hatua hizi ni za kipekee za kurekebisha hali (exceptional intervention) kwa lengo la kurejesha uadilifu, uwazi na imani katika Uongozi wa Michezo Nchini, na si kwa lengo la kuingilia uhuru wa Vyama vya Michezo.

Waziri Makonda amesema "Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuweka mazingira bora ya Maendeleo ya Michezo nchini ili kuhakikisha Tanzania inashiriki kikamilifu na kwa mafanikio katika mashindano ya Kimataifa kama vile Michezo ya Jumuiya ya Madola, Michezo ya Afrika na Michezo ya Olimpiki.

"Ni matarajio yangu kuwa kupitia uamuzi huu, Kamati ya Olimpiki Tanzania itaimarika zaidi na kuweka mazingira bora yatakayowezesha Wanamichezo wetu kufanya vizuri Kimataifa na hatimaye kuliletea Taifa heshima kwa kushinda medali, hususan Medali za Dhahabu ambazo zimekuwa adimu kwa muda mrefu.

"Ninawaomba wadau wote wa michezo kuwa watulivu, kuendelea kushirikiana, na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya Uchunguzi na Uongozi wa muda ili kufanikisha mchakato huu wa marekebisho kwa manufaa ya Taifa."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here