NAIROBI-Serikali ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuunganisha maendeleo ya kikanda, mipango miji pamoja na miundombinu kama nyenzo muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi na ujumuishaji wa kikanda Barani Africa.
Akizungumza katika mjadala wa kitaalamu uliofanyika sambamba na Kongamano la Pili la Miji Afrika (2nd Africa Urban Forum) jijini Nairobi jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Leonard Akwilapo ameeleza kuwa, kanda za maendeleo zina mchango mkubwa katika kurahisisha biashara, usafirishaji na kuunganisha nchi zisizo na bandari na masoko ya kimataifa.
‘’Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza kanda mbalimbali tangu miaka ya 1970 ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa nchi na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,,’’amesema.
Kwa mujibu wa Dkt.Akwilapo, Kanda ya Kati imeendelea kuwa mhimili muhimu wa usafirishaji, ikiunganisha Bandari ya Dar es Salaam na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupitia reli, barabara na njia za majini.8
Amebainisha kuwa, ongezeko la kasi la ukuaji wa miji limeongeza mahitaji ya miundombinu na huduma, huku mahitaji ya usafiri yakiongezeka mara nne ndani ya kipindi cha miaka 20 iliyopita.
‘’Hali hii imeifanya serikali kuongeza uwekezaji katika sekta ya miundombinu na mipango miji ili kukidhi mahitaji hayo,’’ameeleza.




