NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya matumizi ya ofisi hiyo katika mwaka wa fedha 2026/2027, akisisitiza kuwa fedha hizo zitalenga kuimarisha utendaji kazi wa Serikali pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti bungeni jijini Dodoma leo Aprili 17,2026, Waziri Kikwete amesema, kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.4 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku shilingi bilioni 163 zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika tathmini ya utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Waziri huyo amesema,ofisi yake kwa kushirikiana na taasisi zake imepata mafanikio makubwa katika kusimamia rasilimaliwatu na kuboresha mifumo ya kiutumishi serikalini.
Amesema,katika kipindi hicho, jumla ya vibali vya ajira mpya 43,866 vilitolewa, ambapo nafasi 41,500 ziliidhinishwa kwa taasisi zinazolipa mishahara kupitia mfumo wa kielektroniki wa e-Watumishi, huku nafasi 2,366 zikiidhinishwa kwa taasisi zinazojigharamia kupitia mapato ya ndani.
Aidha, madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma 13,551 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17.7 yalihakikiwa na kulipwa.
Vilevile, madai ya watumishi 1,241 waliokoma utumishi wao yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 5.5 yalilipwa baada ya uhakiki.
Katika kuimarisha usimamizi wa taarifa za watumishi, jumla ya taarifa 190,132 zilichambuliwa na kuidhinishwa kupitia mfumo wa e-Watumishi, zikihusisha ajira mpya, mabadiliko ya kada, nyongeza za mishahara pamoja na upandishwaji wa vyeo.
Kwa upande wa uhakiki wa watumishi, Waziri Kikwete amesema, zoezi hilo lilifanyika kwa watumishi 17,432 katika sekta ya afya, likihusisha makao makuu ya wizara pamoja na hospitali za rufaa za mikoa na kanda.
Aidha, katika juhudi za kujenga uwezo wa watumishi, jumla ya watumishi 18,300 kutoka mikoa 13 walipatiwa mafunzo kupitia programu ya “Mobile Clinic” ili kuboresha matumizi ya mfumo wa e-Utendaji na kuongeza ufanisi kazini.
Sambamba na hilo, vibali mbalimbali vilitolewa ikiwemo vibali 611 vya kujaza nafasi za uongozi, vibali 311 vya kukaimu nafasi, vibali 1,345 vya ajira mbadala na vibali 5,469 vya uhamisho wa watumishi, hatua inayolenga kuongeza tija katika utumishi wa umma.
Waziri huyo pia ameeleza kuwa, Serikali imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali, ambapo maboresho ya mifumo ya e-Watumishi, e-Utendaji na Watumishi Portal yamefanyika, ikiwemo kuongeza moduli za mipango ya rasilimaliwatu na kuboresha mazingira ya kuhifadhi taarifa kwa kufunga seva mpya nne.
Katika hatua nyingine, programu ya maboresho ya utumishi wa umma inayolenga wananchi (Citizen Centric Public Service Modernization Programme) imeandaliwa, ikiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za Serikali. Programu hiyo inatarajiwa kugharamiwa kwa fedha za ndani pamoja na ufadhili kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumzia hali ya rasilimaliwatu serikalini, Waziri Kikwete amesema, tathmini iliyofanyika kupitia mfumo wa e-Msawazo imebaini kuwa kuna jumla ya watumishi 655,737 dhidi ya mahitaji halisi ya 930,423, hivyo kuonyesha upungufu wa watumishi 274,686 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Katika kuimarisha maadili na uwajibikaji, Serikali imetoa mafunzo kwa watumishi 23,370 kutoka taasisi 42, pamoja na kutoa elimu ya maadili kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Aidha, huduma za ushauri wa kisheria zilitolewa kwa taasisi 150 kuhusu masuala ya kinidhamu na tafsiri ya sheria za utumishi wa umma.
Kwa upande wa usimamizi wa utendaji kazi, Waziri huyo amesema, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mikataba ya utendaji kazi ulifanyika katika taasisi za umma 256 kupitia mfumo wa e-Utendaji, hatua inayolenga kuongeza uwazi na uwajibikaji serikalini.
Hotuba hiyo pia imegusia jitihada za Serikali katika kutekeleza ahadi zake, ambapo kipindi maalum cha televisheni kilirushwa kuelezea utekelezaji wa siku 100 za ahadi za Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa ujumla, Waziri Kikwete amesisitiza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mifumo, kuongeza ajira, na kuimarisha maadili katika utumishi wa umma ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, zenye tija na zinazokidhi matarajio ya maendeleo ya taifa.
Tags
Bunge la Bajeti
Bunge la Tanzania
Habari
Ofisi ya Rais-Utumishi
Ridhiwani Jakaya Mrisho Kikwete
