DAR-Serikali kupitia Wizara ya Fedha, imewataka watoa Huduma za Fedha nchini kubuni na kuanzisha bidhaa na huduma za fedha zinazoendana na sekta za kiuchumi na kuendelea kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa wajasiriamali na wananchi.
Maaagizo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), wakati akifunga Jukwaa la Pili la Wadau wa Sekta ya Fedha la Mwaka 2026, lililofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Biashara-PSSSF jijini Dar Es Salaam.
Mhe. Munde alieleza kuwa, Serikali itahakikisha kuwa sekta binafsi inashiriki katika masuala yanayohusu sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya fedha pamoja na sekta ya bima ili kuyafikia malengo yaliyopo kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
‘’Uanzishwaji wa uwekezaji wa mitaji ya kibinafsi ambao haufanyiki kwenye soko la hisa la umma (venture capital and private equity) uhusishe sekta binafsi na Umma, na watoa huduma za fedha wabuni na kuanzisha bidhaa ambazo zitawagusa wananchi wa kipato cha chini,’’alisema Mhe. Munde (Mb).
Kwa upande wake Kaimu Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Dionisia Mjema, aliwataka wadau wa sekta ya fedha, wakiwemo benki, kampuni za bima na mifuko ya hifadhi ya jamii, kuendelea kuandaa bidha na huduma za fedha zenye gharama nafuu ili kuwezesha upatikanaji wa mitaji itakayokidhi mahitaji ya shughuli za kijamii na kiuchumi.
Aliongeza kuwa,sekta ya fedha nchini ina jukumu kubwa katika kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, kupitia utoaji wa mitaji nafuu itakayosaidia kukuza shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Katika siku ya pili ya Jukwaa la Pili la Wadau wa Sekta ya Fedha, washiriki walipata mafunzo kupitia mawasilisho yaliyotolewa na wataalam mbalimbali ikiwemo wataalam kutoka Mamlaka ya Bima Tanzania, Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, wataalam kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, huku wakiahidi kuyafanyia kazi maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na viongozi wakuu wa Wizara ya Fedha katika Jukwaa hilo.








