NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) imeipongeza Kampuni ya iTrust Finance Limited kwa kufanikisha utoaji wa hatifungani ya iTrust Bond baada ya kukidhi matakwa yote ya sheria,kanuni na miongozo inayosimamia masoko ya mitaji nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 19, 2026 jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA,CPA Nicodemus Mkama kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utafiti,Sera na Mipango wa mamlaka hiyo, CPA Alfred Mkombo, wakati wa hafla ya uzinduzi wa hatifungani hiyo.
Katika hafla hiyo, CMSA imeeleza kuwa, uzinduzi wa hatifungani hiyo ni hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha na masoko ya mitaji nchini, huku ukiendelea kuongeza wigo wa bidhaa za uwekezaji zinazopatikana kwa wananchi na taasisi mbalimbali.
Hatifungani hiyo ni Programu ya Hatifungani ya Muda wa Kati (Medium-Term Note Programme-MTN) yenye thamani ya shilingi bilioni 100, ambapo awamu ya kwanza inalenga kukusanya shilingi bilioni 15 huku kukiwa na nyongeza ya shilingi bilioni tano kupitia chaguo la ziada.
Kwa mujibu wa CMSA, iTrust Bond imeidhinishwa rasmi baada ya kampuni hiyo kukidhi masharti yote yaliyoainishwa katika Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Sura ya 79 pamoja na Miongozo ya Utoaji wa Hatifungani kwa Umma ya mwaka 2019.
“Napenda kutoa taarifa kwa umma kuwa iTrust Bond ya Kampuni ya iTrust Finance Limited imepata idhini ya CMSA baada ya kukidhi matakwa yote ya sheria, kanuni na miongozo ya utoaji wa hatifungani kwa umma."
Aidha,ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti ya iTrust pamoja na wataalamu wa masoko ya mitaji waliohusika katika kufanikisha mchakato huo, akisema hatua hiyo inaonesha ukuaji wa taaluma na ufanisi ndani ya sekta ya fedha nchini.
CMSA imeeleza kuwa,fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hiyo zitatumika kusaidia utekelezaji wa mkakati wa iTrust wa kukuza biashara ikiwemo utoaji wa mikopo kwa kampuni ndogo na za kati za ujasiriamali (SMEs), hususan zinazomilikiwa au kutoa huduma kwa wanawake na vijana.
Aidha, mamlaka hiyo imesema mpango huo unaendana na Mkakati wa Taifa wa Kuwezesha Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kwa SMEs wa mwaka 2023/24 hadi 2028/29 pamoja na Mpango Mkuu wa Maendeleo wa Sekta ya Fedha wa mwaka 2020/21 hadi 2029/30.
Katika maelezo yake, CMSA imebainisha kuwa, iTrust tayari ina historia nzuri katika masoko ya mitaji baada ya kufanikisha utoaji wa hatifungani za Sukuk 12 zenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 98.1 ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita.
Mamlaka hiyo imesema,wawekezaji wa Sukuk hizo wameendelea kupata mapato ya uwekezaji kwa wakati huku kampuni hiyo ikifanikiwa kulipa hatifungani zote zilizokomaa bila changamoto.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela amesema, uzinduzi wa hatifungani ya iTrust Bond yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 15 unatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kukuza sekta ya masoko ya mitaji nchini pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji kwa wananchi.
Pia, amesema iTrust Finance Limited kuingia kwenye soko la hatifungani ni ishara ya kuendelea kukua kwa imani ya sekta binafsi katika matumizi ya masoko ya mitaji kama chanzo mbadala cha upatikanaji wa fedha za maendeleo.
Amesema, bidhaa hiyo mpya ya kifedha itasaidia kuongeza kina cha soko la mitaji nchini kwa kutoa chaguo zaidi kwa wawekezaji wanaotafuta uwekezaji wenye mapato ya uhakika na hatari ndogo.
Kwa mujibu wa DSE, kuongezeka kwa utoaji wa hatifungani za kampuni binafsi kunasaidia kupanua ushiriki wa wananchi katika sekta ya uwekezaji huku pia kukichochea ukuaji wa uchumi kupitia upatikanaji wa mitaji kwa biashara na miradi ya maendeleo.
Vilevile amesema, hatua hiyo inaonesha namna masoko ya mitaji yanavyoendelea kuwa mhimili muhimu wa kuchochea maendeleo ya sekta ya fedha nchini, huku akizihimiza taasisi nyingine kutumia fursa ya masoko ya mitaji kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kupanua biashara na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Faiz Arab amesema,kampuni hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya fedha kupitia bidhaa bunifu na matumizi ya teknolojia.
Amesema,wawekezaji wataweza kuwekeza katika hatifungani hiyo kupitia mfumo wa kidijitali wa iTrust App, programu itakayowawezesha wananchi kuwekeza kwenye hatifungani,hisa na mifuko ya uwekezaji kwa urahisi kupitia simu za mkononi.
Kwa mujibu wa iTrust, hatifungani hiyo itatoa riba ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka minne, huku riba ikilipwa kila baada ya miezi mitatu bila kukatwa kodi ya zuio (withholding tax).
Kiwango cha chini cha uwekezaji kimewekwa kuwa shilingi 500,000 ili kutoa fursa kwa wawekezaji binafsi na taasisi kushiriki kwa urahisi katika mpango huo.
Aidha, hatifungani hiyo imefunguliwa rasmi kuanzia Mei 18 hadi Juni 12,2026 na baadae itaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua itakayowaruhusu wawekezaji kununua na kuuza dhamana hizo katika soko la upili.
CMSA imetumia hafla hiyo kutoa wito kwa Watanzania kutumia masoko ya mitaji kama njia ya kukuza uchumi wao binafsi pamoja na kushiriki katika maendeleo ya taifa kupitia uwekezaji katika bidhaa mbalimbali za kifedha.
