DAR-Kampuni ya iTrust Finance Limited imezindua rasmi hatifungani yake, ikiwa ni hatifungani ya kwanza nchini kutolewa na kampuni wakala wa soko la hisa na msimamizi wa mifuko ya uwekezaji nchini Tanzania.
Uzinduzi huo umeanza na awamu ya kwanza ya programu hiyo inayolenga kukusanya Shilingi bilioni 15, ikiwa na nyongeza ya Shilingi bilioni 5 kupitia chaguo la ziada, huku wawekezaji wakitarajiwa kupata riba shindani ya asilimia 13 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka minne.
Riba ya hatifungani hiyo italipwa kila baada ya miezi mitatu bila kukatwa kodi(withholding tax), jambo linalolenga kuwapa wawekezaji mapato ya uhakika na yanayotabirika.
Hatifungani hiyo ijulikanayo kama iTrust Bond, ambayo imeidhinishwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), ilifunguliwa rasmi tarehe 18 Mei 2026 na itafungwa tarehe 12 Juni 2026. Aidha, itaorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), hatua itakayowawezesha wawekezaji kuuza na kununua hatifungani hiyo katika soko la upili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, iTrust ilieleza kuwa muundo wa hatifungani hiyo umeandaliwa kwa namna inayowavutia wawekezaji wa aina mbalimbali, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwekwa kuwa Shilingi 500,000 ili kutoa nafasi kwa wawekezaji binafsi na taasisi kushiriki kwa urahisi.
Kampuni hiyo ilibainisha kuwa hatifungani hiyo ina manufaa mbalimbali ikiwemo riba shindani yenye kiwango kisichobadilika, msamaha wa kodi ya zuio kwenye riba pamoja na kuongeza fursa ya uwekezaji kupitia dhamana za mapato yasiyobadilika (fixed income investments).
Pia ilieleza kuwa muda mfupi wa ukomavu wa miaka minne pamoja na mfumo wa malipo ya kila robo mwaka vinaifanya iTrust Bond kuwa mbadala wenye mvuto ukilinganishwa na dhamana za kawaida za serikali.
Fedha zitakazopatikana kupitia utoaji wa hatifungani hiyo zitatumika katika kutekeleza mipango mbalimbali ya kimkakati ikiwemo kuongeza uwezo wa utoaji mikopo, kuwekeza katika majukwaa ya kidijitali ya kisasa pamoja na kuimarisha mtaji wa uendeshaji wa kampuni kwa ajili ya kukuza shughuli zake.
Katika kurahisisha usajili wa iTrust Bond, Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance Limited, Bw. Faiz Arab, alionesha namna rahisi ya kuwekeza kupitia uzinduzi wa programu ya simu ya iTrust App.
Programu hiyo ya kipekee itawawezesha watumiaji kuwekeza katika hatifungani, hisa na mifuko ya uwekezaji huku wakifuatilia uwekezaji wao wote katika sehemu moja.
iTrust Finance Limited ni taasisi ya huduma za kifedha ya daraja la pili (Tier 2) iliyoidhinishwa na kusimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na CMSA.
Kampuni hiyo hutoa huduma mbalimbali za kifedha zikiwemo uwakala wa soko la hisa, ushauri wa uwekezaji, usimamizi wa mifuko ya uwekezaji pamoja na huduma za mikopo ya kawaida na inayozingatia misingi ya Shariah kupitia kitengo chake cha Imaan Finance.
Kwa kuzingatia nafasi yake kubwa sokoni na kuendelea kujijengea sifa kama mshirika wa kuaminika katika uwekezaji, iTrust inalenga kutumia programu hii kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya fedha nchini huku ikiunga mkono ukuaji wa uchumi shirikishi.
Wawekezaji wanaweza kupata taarifa zaidi na kuwasilisha maombi ya kuwekeza katika hatifungani hiyo kupitia majukwaa ya kidijitali ya iTrust ikiwemo aplikesheni, tovuti na mfumo wa mtandaoni wa kampuni hiyo.