NA ARON MSIGWA
Nairobi
JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Majeshi ya Ulinzi ya nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yamehitimisha kwa mafanikio zoezi la 14 la pamoja la Vituo vya Uamrishaji vya Kijeshi lijulikanalo kama Ushirikiano Imara 2026 jijini Nairobi, Kenya.


Hafla ya kufunga zoezi hilo imehudhuriwa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Salum Haji Othman, aliyemwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob John Mkunda.
Zoezi hilo kubwa la kijeshi limewakutanisha washiriki zaidi ya 400 kutoka Kenya, Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, likiwa na lengo la kuimarisha utayari, mshikamano na uwezo wa vikosi vya ulinzi na usalama vya nchi wanachama wa EAC katika kukabiliana na changamoto na matishio ya kiusalama yanayolikabili eneo la Afrika Mashariki.
Akizungumza wakati wa kufunga zoezi hilo, Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kenya, Soipan Tuya, amesisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa EAC kuendelea kuimarisha ushirikiano, mshikamano na maandalizi ya pamoja katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama, majanga mbalimbali pamoja na changamoto zinazoweza kuhatarisha amani na utulivu wa kikanda.
“Kupitia zoezi hili, tumeimarisha uwezo wetu wa kukabiliana na majanga, kubaini mapema changamoto zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati sahihi ya kukabiliana nazo,” amesema Waziri Tuya.
Aidha, amesema ameridhishwa na mafanikio yaliyopatikana kupitia mafunzo hayo na kuwapongeza Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwezesha utekelezaji wa zoezi hilo muhimu.
“Ninayo furaha kueleza kuwa malengo yote ya mafunzo haya yamefikiwa kwa kiwango kikubwa. Nawashukuru Wakuu wa Nchi za EAC kwa kuwezesha zoezi hili na nawapongeza washiriki wote kwa kuendelea kulinda amani, utulivu na uhuru wa nchi zetu,” amesisitiza.
Zoezi la Ushirikiano Imara 2026 lilijikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo Operesheni za Kusaidia Amani (PSO), mapambano dhidi ya ugaidi (CT), kukabiliana na uharamia baharini (CP) pamoja na usimamizi wa maafa (DM).
Katika kipindi cha mafunzo hayo, vikosi kutoka Tanzania, Kenya, Burundi, Rwanda, Uganda, Somalia na Sudan Kusini vilionesha umahiri mkubwa katika mafunzo ya mawasiliano ya kimkakati, ubadilishanaji wa taarifa za kiusalama, uratibu wa operesheni, doria katika maeneo ya mijini pamoja na mbinu za utendaji katika mazingira hatarishi.
Kwa upande wa Tanzania, zoezi hilo lilihusisha maafisa kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Magereza, Wizara pamoja na taasisi mbalimbali za kiraia. Washiriki hao walionesha kiwango cha juu cha taaluma, nidhamu na uwezo wa kiutendaji sambamba na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kulinda amani na usalama.
Aidha, zoezi hilo limeendelea kuimarisha mipango ya pamoja ya kuzuia migogoro, kuongeza utayari wa kukabiliana na majanga pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji wa misaada ya kibinadamu, upangaji na utekelezaji wa operesheni za pamoja zinazohusisha vyombo vya ulinzi na wadau wa kiraia katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Hafla ya kufunga zoezi hilo pia imehudhuriwa na Brigedia Jenerali Maneno Almasi Mabakila kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambaye alikuwa Msimamizi Mkuu wa zoezi hilo la 14 (Chief Umpire) na Kiongozi wa Kikundi cha Tanzania, sambamba na viongozi mbalimbali na maafisa waandamizi wa majeshi kutoka nchi wanachama wa Afrika Mashariki.



