NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeishauri Serikali kutoa mtaji wa Shilingi bilioni 300 kwa Bohari ya Dawa (MSD) pamoja na kulipa deni la Shilingi bilioni 302 linalodaiwa na taasisi hiyo, hatua itakayosaidia kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya nchini.
Ushauri huo umetolewa leo Mei 11, 2026 bungeni jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt.Zeyana Abdallah wakati akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27.
"Serikali itoe mtaji wa shilingi bilioni 300 kwa Bohari ya Dawa (MSD) ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa bidhaa za afya, kusaidia uwekezaji kwenye viwanda na kuongeza uwezo wa uhifadhi bidhaa za afya na kujenga maghala ya kutosha."
Amesema, kukosekana kwa mtaji huo kunasababisha Bohari ya Dawa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi kwa ufanisi.
"Serikali ilipe deni inalodaiwa na Bohari ya Dawa lenye thamani ya shilingi bilioni 302 kwa mchanganuo wa shilingi bilioni 46.4 kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya Wizara ya Afya, shilingi bilioni 83.1 kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, na shilingi bilioni 172.7 za miradi misonge."
Amesema, ni muhimu madeni hayo yakalipwa ili kulinda mnyororo wa ugavi na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa utoshelevu.
Dkt.Zeyana amesema,Serikali inapaswa kuongeza uwekezaji katika mifumo ya kinga na kuzijengea uwezo taasisi zake ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa,hatua hiyo itaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030.
Katika eneo la rasilimali watu, kamati hiyo imeitaka Serikali kuendelea kutoa vibali vya ajira kwa kada zenye upungufu mkubwa katika vituo vya kutolea huduma za afya, huku ikisisitiza umuhimu wa kuzingatia mahitaji halisi ya taasisi pamoja na kuwapa kipaumbele wataalam wanaojitolea katika hospitali mbalimbali nchini.
Aidha,kamati imependekeza kuongezwa kwa ufadhili wa masomo kwa wataalam wa afya ili waweze kupata mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Dkt.Zeyana, hatua hiyo itasaidia kuongeza wataalam wenye ujuzi wa hali ya juu na kuboresha utoaji wa huduma za afya nchini.
“Tunaitaka Serikali kuongeza ufadhili wa masomo kwa wataalam wa afya ili kupata mafunzo ya ubingwa na ubingwa bobezi ndani na nje ya nchi, hatua itakayoongeza wataalam wenye ujuzi wa hali ya juu katika sekta ya afya,”amesema Dkt.Zeyana.
Pamoja na ushauri huo,kamati imeipongeza Serikali kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika sekta ya afya, ikiwemo kuanza kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, kuimarishwa kwa hospitali za rufaa za mikoa na kanda pamoja na mpango wa ujenzi wa Hospitali mpya ya Taifa ya Muhimbili.
Kamati hiyo pia imeeleza kuridhishwa na hatua ya Serikali kuendelea kununua vifaa tiba vya kisasa, ikiwemo mashine za PET CT Scan, MRI, Angio Suite na Mammography ambazo zimeendelea kusaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu na kuokoa fedha za kigeni.
Dkt.Zeyana amesema kuwa,hakuna maendeleo ya kweli yanayoweza kupatikana bila uwekezaji madhubuti katika sekta ya afya, akisisitiza kuwa afya bora ya wananchi ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya taifa.
Vipaumbele 11 vya Afya
Awali, Waziri wa Afya,Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameliambia Bunge kuwa, wizara hiyo inatarajia kutekeleza vipaumbele 11 vya kwa mwaka wa fedha 2026/27, vikilenga kuimarisha sekta ya afya nchini kupitia maboresho ya huduma za tiba, kinga, miundombinu, matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa wataalamu wa afya.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27, Waziri Mchengerwa amesema, hatua hiyo inalenga kuongeza ubora wa huduma za afya kwa wananchi na kuhakikisha mfumo wa afya unakuwa imara, jumuishi na unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Waziri Mchengerwa amesema,Serikali itaendelea kuimarisha ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote ili kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa. Lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye kuzingatia weledi wa kitaaluma katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.
Aidha, Wizara imeweka mkazo katika kuimarisha mfumo wa ugharamiaji wa huduma za afya nchini kupitia utekelezaji endelevu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Mfumo huo unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wananchi wengi zaidi huku ukipunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia.
Katika kukuza sekta ya uzalishaji wa bidhaa za afya, Serikali imepanga kuwezesha na kuharakisha uwekezaji wa viwanda vya ndani kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji wa bidhaa za afya. Mpango huo unalenga kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuimarisha uwezo wa taifa kujitosheleza katika mahitaji muhimu ya afya.
Wizara pia imeeleza dhamira yake ya kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za afya.
Matumizi hayo yatasaidia kuongeza ufanisi, kurahisisha upatikanaji wa taarifa za afya, kuboresha usimamizi wa huduma na kuongeza uwazi katika sekta hiyo.
Katika eneo la kinga dhidi ya magonjwa, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Magonjwa yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na mlipuko wa magonjwa, magonjwa yaliyopewa kipaumbele kitaifa pamoja na kuimarisha afua za lishe na usafi wa mazingira kwa lengo la kuzuia athari za kiafya kwa jamii.
Kwa upande wa afya ya uzazi, mama na mtoto, Wizara imepanga kuimarisha huduma hizo kwa kuhakikisha watoto wachanga na watoto walio chini ya miaka mitano wanapatiwa huduma bora zinazookoa maisha na kuboresha ustawi wao.
Hatua hiyo inaendana na juhudi za kupunguza vifo vya wajawazito, watoto wachanga na watoto wenye umri mdogo.
Katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wataalamu wa afya, Serikali imeweka mkazo katika kuimarisha upatikanaji na maendeleo ya watumishi wa sekta hiyo katika kada mbalimbali.
Aidha, hatua madhubuti zitaendelea kuchukuliwa kupambana na ubingwa bobezi kwa lengo la kuongeza wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu nchini.
Wizara pia imeainisha umuhimu wa kuimarisha huduma za tiba asili na tiba mbadala kwa kuzingatia miongozo, usalama na ubora wa huduma hizo.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanaotumia tiba hizo wanapata huduma salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Katika mapambano dhidi ya magonjwa mbalimbali, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za tiba dhidi ya magonjwa pamoja na kuendeleza huduma za ubingwa na ubingwa bobezi nchini.
Sambamba na hilo, juhudi za kuendeleza tiba utalii zitapewa kipaumbele ili kuvutia wagonjwa kutoka nje ya nchi na kuongeza mchango wa sekta ya afya katika uchumi wa taifa.
Kwa upande mwingine, Wizara imeweka kipaumbele katika kuimarisha huduma za afya ya akili pamoja na huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Mpango huo unakusudia kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalumu na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa ujumla, vipaumbele hivyo vinaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha sekta ya afya nchini kwa kuwekeza katika kinga, tiba, teknolojia, rasilimali watu na miundombinu.
Wachambuzi wa masuala ya afya wanaeleza kuwa utekelezaji mzuri wa mikakati hiyo unaweza kuongeza ubora wa maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Shilingi trilioni 1.8
Katika hatua nyingine, Waziri Mchengerwa ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 1.8 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Afya katika mwaka wa fedha 2026/27.
Amefafanua kuwa,kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.148 sawa na asilimia 64 ya bajeti hiyo zitatumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 789.45 ni fedha za ndani huku shilingi bilioni 358.56 zikitokana na washirika wa maendeleo.
Aidha, wizara hiyo imepanga kutumia shilingi bilioni 652.236 kwa matumizi ya kawaida, ambapo shilingi bilioni 516.323 zitatumika kwa mishahara ya watumishi wa afya na shilingi bilioni 135.913 kwa matumizi mengineyo.
Waziri Mchengerwa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Wizara ya Afya kupata fedha nyingi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hatua aliyosema imeiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika zinazotoa huduma za matibabu kwa gharama nafuu.
Mwisho, Waziri huyo ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti hiyo akisema utekelezaji wake utasaidia kutekeleza vipaumbele 11 vya wizara hiyo vinavyolenga kuifanya Tanzania kuwa mfano wa utoaji bora wa huduma za afya barani Afrika.
