MOROGORO-Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Zuzu, Dodoma, unatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 18, 2026.
Akizungumza Mei 20, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo katika mikoa ya Morogoro na Dodoma, Bw. Twange amesema mradi huo ni muhimu kwa kuwa unasafirisha umeme unaozalishwa moja kwa moja kutoka katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere ambao unapita Chalinze hadi Dodoma.
Amesema utekelezaji wa mradi huo unaenda sambamba na upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Chalinze na Zuzu, Dodoma, ambapo kukamilika kwake kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa ajili ya shughuli za uwekezaji pamoja na kuongeza fursa mbalimbali za kiuchumi nchini.Amesema Serikali Chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha Shilingi Bil 514 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huo ambao utachochea shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii kuendana na kasi ya ongezeko la mahitaji.
“Leo tumefanya ukaguzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma. Njia hii ni muhimu kwa kuwa inaongeza uwezo wa kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kwenda kwa watumiaji mbalimbali. Idadi ya watu imeongezeka na shughuli za kiuchumi zimeongezeka hivyo tumeingia makubaliano sasa mradi huu utakamilika Agosti 18, 2026,” alisisitiza Bw. Twange.
Ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa huku akimtaka mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
“Tumekubaliana kuongeza wataalamu na vifaa vya kutosha ili kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya muda ulioainishwa,” ameongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mradi, Mhandisi Newtone Lingstone, amesema mradi huo wenye urefu wa kilometa 345 Kutoka Chalinze hadi Dodoma unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania, huku kazi za upanuzi wa vituo vya kupokea na kupoza umeme vya Chalinze na Dodoma zikiendelea vizuri.





