MOROGORO-Wananchi wa Kijiji cha Parakuyo kilichopo Kata ya Parakuyo Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wametakiwa kuacha kuwatumia watoto katika shughuli za kuchunga mifugo,kwani kwa kufanya hivyo kutachagiza kupoteza ndoto zao hususani za kimasomo.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Ushirikishwaji Jamii wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini,Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,SSP Juma Bonza alipokuwa akitoa elimu ya kuzuia uhalifu wa mifugo pamoja na kusikiliza kero za wafugaji na wakulima wilayani humo, ambapo amesema kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwa kipaumbele katika kutimiza ndoto za watoto wao na sio kuwapa majukumu ya kuchunga mifugo.
Aidha, SSP Bonza amesema kuwa katika kutokomeza wizi wa mifugo, ni vyema askari wakawashirikisha wafugaji wenyewe katika kufanya misako mbalimbali itakayochangia kutokomeza wizi wa mifugo kwa njia ya kuswagwa maporini.
Kwa upande wake Mkaguzi Kata wa kata hiyo, Mkaguzi wa Polisi,INSP Zuneri Shubeit ameshukuru kwa elimu hiyo na kuahidi kuyasimamia maelekezo yote yaliyotolewa, huku akiongeza kwa kusema kuwa ni vyema ukaguzi wa mabucha na machinjio ukaongezwa katika kubaini wanao nunua na kuuza nyama za wizi katika kata hiyo.
