Mwinjilisti Dkt.Temba awahimiza viongozi wa umma kumtanguliza Mungu na uzalendo kwanza

PWANI-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt.Alphonce Temba ambaye amewahi kuishi na kufanya ziara za kiinjilisti katika zaidi ya mataifa 12 duniani, ametoa wito kwa Watanzania wote waliopata nafasi za kulitumikia taifa katika ofisi za umma kuhakikisha wanamtanguliza Mungu mbele, uadilifu na uzalendo wa kweli katika utendaji wao wa kazi.
Akizungumza leo Mei 16,2026 Dkt.Temba amesema,viongozi na watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa nafasi walizopewa ni dhamana ya muda mfupi mbele ya historia na jamii, hivyo wanapaswa kuacha alama njema zitakazokumbukwa na vizazi vijavyo.

“Binadamu amepewa muda mfupi sana wa kulitumikia taifa. Nafasi za uongozi si za milele, hivyo kila mmoja anatakiwa kuhakikisha anatumia nafasi yake kwa haki, uadilifu na kwa kumcha Mungu,”amesema Dkt.Temba.

Amegusia pia umuhimu wa haki katika mfumo wa Mahakama nchini, akieleza kuwa baadhi ya majaji wameendelea kujijengea heshima kubwa mbele ya wananchi kutokana na misimamo yao ya kusimamia haki bila kuyumbishwa na mashinikizo mbalimbali.

Akimtaja mmoja wa majaji anaowaheshimu kwa uadilifu wake, Dkt.Temba amemzungumzia Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi, Jaji E. I. Laitaita akisema ni miongoni mwa majaji wanaotambulika kwa misimamo madhubuti katika utoaji wa maamuzi ya kesi zenye utata mkubwa.

Kwa mujibu wa Dkt.Temba, Jaji Laitaita amejijengea sifa ya kuwa mwamuzi makini anayesisitiza ushahidi wa kweli na haki kwa pande zote, jambo ambalo limewafanya mawakili wengi wanaofika mbele yake kujiandaa kwa umakini mkubwa wanapotetea wateja wao.

Amesema,baadhi ya mawakili waliowahi kufanya kazi au kufundishwa chini ya jaji huyo wamekuwa wakitumia maamuzi yake kama rejea muhimu katika kushughulikia migogoro mbalimbali ya ardhi katika mabaraza ya wilaya na mahakama nyingine nchini.

Dkt.Temba ametoa mfano wa Shauri la Rufaa Na. 25463 la mwaka 2024, ambalo lilihusisha mgogoro wa mauzo ya ardhi kati ya watu saba waliouziwa eneo moja na muuzaji mmoja.

Katika shauri hilo, sita kati ya wanunuzi hao waliungana dhidi ya mnunuzi mmoja aliyekuwa akidai haki yake.

Katika hukumu yake, Jaji Laitaita alinukuliwa akieleza kuwa,biashara ya kuuza na kununua ardhi ni makubaliano yanayowahusu zaidi muuzaji na mnunuzi wenyewe, huku mashahidi, viongozi wa mitaa, vijiji au hata mawakili wakibaki kuwa mashahidi wa tukio na si wamiliki wa ukweli wa msingi kuhusu umiliki wa eneo husika.

Aidha, hukumu hiyo ilisisitiza kuwa kila mnunuzi wa ardhi anapaswa kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kufanya malipo au kukamilisha biashara, ili kujiridhisha kuwa eneo halina mgogoro, halijawekwa rehani na muuzaji ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo.

Mbali na masuala ya Mahakama, Dkt.Temba pia aliigusia sekta ya miundombinu na usimamizi wa bandari kavu nchini, ambapo aliitaka Menejimenti ya Mamlaka husika pamoja na taasisi za usimamizi wa mazingira kuhakikisha zinafanya maamuzi yatakayolinda maslahi mapana ya taifa.

Aliwataka viongozi wa taasisi hizo kuangalia upya utoaji wa vibali vya ujenzi wa bandari kavu katika maeneo mbalimbali, akieleza kuwa ongezeko holela la miradi hiyo linaweza kuongeza changamoto za msongamano na athari kwa jamii.

Kwa mujibu wake, Bandari Kavu ya Kwala ina uwezo mkubwa wa kupunguza msongamano wa malori ndani ya Jiji la Dar es Salaam na kusaidia kuboresha mfumo wa usafirishaji wa mizigo nchini endapo itatumika kikamilifu kwa mipango ya kitaifa.

“Hakuna sababu ya kuwa na utitiri wa bandari kavu kila kona wakati taifa tayari lina miundombinu yenye uwezo wa kuhudumia mahitaji yaliyopo. Tunapaswa kuangalia maslahi ya taifa kwanza,”amesema.

Kauli za Dkt.Temba zimeendelea kupokelewa kwa mitazamo tofauti katika jamii, huku baadhi ya wananchi na wadau wakizitafsiri kama wito wa kuimarishwa kwa uwajibikaji, maadili ya uongozi na usimamizi bora wa rasilimali za taifa, ambapo DIRAMAKINI tunaendelea kufuatilia hoja zake kwa makini ili kupata taarifa kwa kina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here