NHC yavutia wananchi na wadau Maonesho ya Nne ya Mbeya Expo 2026

MBEYA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki Maonesho ya Nne ya Mbeya Expo 2026 yanayoendelea kufanyika jijini Mbeya kuanzia Mei 22 hadi Mei 30,mwaka huu wa 2026.
Maonesho hayo yalifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Mheshimiwa Beno Malisa ambapo yanawakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za Serikali na zisizo za Serikali kwa lengo la kuhamasisha biashara, uwekezaji pamoja na maendeleo ya uchumi wa kikanda.

Tukio hilo linafanyika katika viwanja vya lililokuwa Soko la Uhindini jijini Mbeya, ambapo washiriki mbalimbali wanatumia fursa hiyo kutangaza huduma, bidhaa na miradi yao kwa wananchi na wawekezaji kutoka maeneo tofauti ya nchi.
Shirika la Nyumba la Taifa linatumia maonesho hayo kuendelea kutangaza na kuuza miradi yake mbalimbali ya makazi na biashara inayotekelezwa katika maeneo tofauti nchini, ikiwa ni sehemu ya juhudi za shirika hilo katika kukuza sekta ya nyumba na uwekezaji wa majengo ya kisasa.

Miongoni mwa miradi inayotangazwa na NHC katika maonesho hayo ni pamoja na mradi wa 711, Kijichi Residence, Medeli III iliyopo Dodoma, Mkwakwani Plaza, Iringa Commercial Complex, Uluguru Plaza pamoja na Tabora Plaza.
Kupitia ushiriki huo, wananchi wanaopata nafasi ya kutembelea banda la NHC wanapatiwa elimu kuhusu fursa za uwekezaji katika sekta ya nyumba, taratibu za upatikanaji wa nyumba pamoja na maeneo ya biashara yanayosimamiwa na shirika hilo.

Kauli mbiu ya Maonesho ya Mbeya Expo mwaka huu ni “Kujenga Uchumi wa Kikanda Kupitia Biashara na Uwekezaji,” ikiwa inalenga kuhamasisha ushirikiano wa kiuchumi, kuvutia wawekezaji na kuongeza mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya mikoa na taifa kwa ujumla.
Aidha,washiriki wa maonesho hayo wameeleza kuwa tukio hilo linaendelea kuwa jukwaa muhimu la kukuza biashara na kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za umma, sekta binafsi pamoja na wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali za maendeleo na uwekezaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here