NA DIRAMAKINI
RAIS wa Marekani Donald Trump ametangaza kuahirisha shambulio la kijeshi dhidi ya Iran lililokuwa limepangwa kufanyika kesho Mei 19,2026 baada ya viongozi wakuu wa Mashariki ya Kati kuingilia kati na kusisitiza kupewa nafasi kwa mazungumzo ya kidiplomasia.
Kupitia ujumbe uliosambaa katika mitandao ya kijamii na kuhusishwa na Ikulu ya Marekani, Trump amesema amepokea maombi kutoka kwa Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman pamoja na Rais wa Falme za Kiarabu (UAE), Mohammed bin Zayed Al Nahyan waliomtaka kusitisha kwa muda hatua ya kijeshi dhidi ya Iran ili kutoa nafasi kwa mazungumzo yanayoendelea.
Katika taarifa hiyo, Trump amesema viongozi hao wa Ghuba wameonesha imani kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa kati ya Marekani na Iran, makubaliano ambayo yatakuwa na manufaa kwa Marekani, Mashariki ya Kati pamoja na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla.
“Majadiliano makubwa yanaendelea hivi sasa, na kwa maoni yao kama viongozi wakubwa na washirika wetu, makubaliano yanaweza kufikiwa,” imesomeka sehemu ya ujumbe huo.
Trump pia amesisitiza kuwa,sehemu muhimu ya makubaliano hayo ni kuhakikisha Iran haitamiliki silaha za nyuklia, suala ambalo limeendelea kuwa chanzo kikuu cha mvutano kati ya Tehran na Washington kwa miaka mingi.
Katika hatua hiyo ya kusitisha mashambulizi, Trump amesema amemuelekeza Waziri wa Ulinzi wa Marekani,Pete Hegseth, Mkuu wa Majeshi ya Pamoja,Jenerali Daniel Caine pamoja na vikosi vya kijeshi vya Marekani kuahirisha operesheni hiyo ya kijeshi iliyokuwa imepangwa dhidi ya Iran.
Hata hivyo,ameonya kuwa jeshi la Marekani limeendelea kuwa katika hali ya utayari wa juu na linaweza kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran kwa muda mfupi iwapo mazungumzo hayo hayatatoa matokeo yanayokubalika kwa Marekani.
Aidha,kauli hiyo imeongeza taharuki mpya duniani huku wachambuzi wa siasa za kimataifa wakieleza kuwa,hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Iran inaweza kuathiri usalama wa eneo lote la Mashariki ya Kati pamoja na uchumi wa dunia, hasa katika sekta ya mafuta na biashara ya kimataifa.
Kwa muda mrefu, Marekani na Iran zimekuwa katika mvutano mkubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo Washington imekuwa ikiitaka Tehran kusitisha shughuli zinazohusishwa na urutubishaji wa uranium kwa madai kuwa zinaweza kutumika kutengeneza silaha za nyuklia. Iran imekuwa ikikanusha madai hayo na kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi ya amani pekee.
Hatua ya viongozi wa Qatar, Saudi Arabia na UAE kuingilia kati inaonekana kuashiria hofu ya mataifa ya Ghuba juu ya uwezekano wa kuzuka kwa vita kubwa ambavyo vinaweza kuvuruga usalama wa eneo hilo pamoja na shughuli za kiuchumi.
Mpaka sasa, hakuna tamko rasmi lililotolewa na serikali ya Iran kuhusu kauli hiyo ya Trump, huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mazungumzo hayo ambayo yanaweza kuamua hatima ya usalama wa Mashariki ya Kati katika siku zijazo.
