Waziri wa Fedha Balozi Omar ashiriki Mkutano wa Uwili kati ya Tanzania na Rwanda

KIGALI-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameshiriki Mkutano wa Uwili (bilateral meeting) kati ya Tanzania na Rwanda, ulioongizwa na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), uliojadili namna ya nchi hizo mbili zinavyoweza kushirikiana katika ujenzi wa miundombinu na biashara ya nishati kwa faida ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo umefanyika Kando ya Mkutano wa Pili wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA) unaofanyika jijini Kigali, nchini Rwanda.

Kwa upande wa Rwanda, Mkutano huo uliongozwa na Waziri wake wa Miundombinu, Mhe. Dkt. Jimmy Gasore, ambapo pamoja na mambo mengine, wamejadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya nishati kati ya Tanzania na Rwanda, katika sekta za umeme, mafuta na gesi asilia.
Pia viongozi hao wamegusia utekelezaji wa miradi ya kikanda ya umeme ikiwemo mradi wa Rusumo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 80 pamoja na mradi wa Nsongezo unaotarajiwa kuzalisha megawati 39 katika Mto Kagera.

Aidha, Mawaziri hao wamejadili kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Tanzania na Rwanda, unaotarajiwa kusainiwa kesho Mei 19, 2026 hatua itakayoimarisha zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya nishati ya umeme, mafuta, gesi asilia pamoja na kufanya biashara ya nishati ya umeme kati ya Mataifa hayo mawili.

Akihitimisha Mkutano huo, Waziri wa Fedha aliipongeza nchin ya Rwanda kwa hatua kubwa iliyopiga kimaendeleo na kwamba ushirikiano huo wa kiuchumi unaojengwa sasa utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi hizo mbili katika kuwaletea wananchi Maendeleo.
Ujumbe huo wa Tanzania pia umemjumuisha Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe. Seif Kombo Pandu, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Felchesmi Mramba, Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Dkt. Habib Kambanga pamoja na wataalam wengine kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here