Ruvuma yapokea majiko banifu 7,648 kwa bei ya ruzuku

RUVUMA-Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, leo Mei 25, 2026 amepokea rasmi mradi wa uuzaji na usambazaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kupitia kampuni ya Burn Manufacturing Company Limited.
Mradi huo unalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kupitia usambazaji wa majiko banifu yenye teknolojia ya kisasa kwa gharama nafuu kutokana na ruzuku inayotolewa na Serikali.

Akizungumza wakati wa kupokea mradi huo, Mkuu wa Mkoa ameipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati safi ya kupikia nchini, akieleza kuwa majiko banifu yana mchango mkubwa katika kuboresha afya za wananchi pamoja na kulinda mazingira.
Amesema,matumizi ya majiko hayo yatasaidia kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa usio salama, ikiwemo moshi unaosababisha madhara ya kiafya kwa watumiaji, hususan wanawake na watoto.

Mheshimiwa Ahmed Abbas Ahmed pia amepongeza ubora wa majiko hayo, akibainisha kuwa yametengenezwa kwa viwango vya hali ya juu pamoja na kuwa na muonekano mzuri unaovutia na utakaowashawishi wananchi kuyatumia kwa wingi.

Aidha, amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia nchini, hatua ambayo inaendelea kusaidia wananchi kupata huduma bora za nishati kwa gharama nafuu.

Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa REA kuendelea kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wengi wanatumia nishati safi na salama.
Amesema,Serikali ya Mkoa wa Ruvuma imepokea mradi huo kwa mikono miwili na ipo tayari kutoa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanikiwa na kuwafikia wananchi walengwa katika maeneo yote yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, mwakilishi wa REA, Ndugu Aziz Abbu amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Amesema,mradi huo utatekelezwa katika wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma ambazo ni Mbinga, Namtumbo, Nyasa, Songea na Tunduru, ambapo jumla ya majiko banifu 7,648 yatasambazwa katika mkoa mzima.

Amefafanua kuwa,kila wilaya itapata majiko 1,530 isipokuwa wilaya za Songea na Tunduru ambazo kila moja itapata majiko 1,529.

Aidha,amesema bei halisi ya jiko moja ni Shilingi 62,261.32, lakini Serikali imetoa ruzuku ya asilimia 80 sawa na Shilingi 49,809.06, hivyo mwananchi atanunua jiko hilo kwa Shilingi 12,452.26 pekee kwa kutumia Kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Naye mwakilishi wa kampuni ya Burn Manufacturing Company Limited, Ndugu John Mtui amesema majiko hayo yametengenezwa kwa teknolojia ya kisasa inayowezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa huku yakipunguza moshi unaotokana na matumizi ya kuni au mkaa kwa zaidi ya asilimia 81.
Ameongeza kuwa,matumizi ya kuni hupungua kwa zaidi ya asilimia 71, jambo ambalo litasaidia kupunguza gharama za matumizi ya nishati kwa wananchi pamoja na kuhifadhi mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here