NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa msimu wa Kipupwe wa kipindi cha Juni hadi Agosti, mwaka 2026 unatarajiwa kuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi nchini, huku mwezi Julai ukitajwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi katika baadhi ya maeneo.
Hayo yameelezwa leo Mei 25,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a wakati akitoa taarifa ya mwenendo wa hali ya hewa kwa kipindi hicho.Amesema,hali ya hewa katika maeneo mbalimbali ya nchi itatofautiana kulingana na jiografia na mifumo ya upepo inayotarajiwa kutawala kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini pamoja na Nyanda za Juu Kusini-Magharibi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi, tofauti na maeneo ya ukanda wa pwani na yale ya katikati ya nchi ambayo yatakuwa na hali ya joto kiasi ikichanganyika na vipindi vya baridi ya wastani.
Ameeleza kuwa,maeneo ya pwani ya kaskazini na kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku baadhi ya maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuhudia hali ya hewa kushuka hadi chini ya nyuzi joto 10 za sentigredi, jambo ambalo linaweza kuongeza athari za kiafya kwa baadhi ya wananchi.
Katika tathmini hiyo ya hali ya hewa, TMA pia imebainisha kuwa msimu huo utatawaliwa na upepo kutoka Kusini Mashariki wenye nguvu iliyopungua kidogo ukilinganishwa na vipindi vya kawaida, ingawa kutakuwepo vipindi vya upepo mkali zaidi katika miezi ya Juni na Julai, hususan katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi pamoja na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.
Dkt.Chang'a ameeleza kuwa,licha ya msimu wa Kipupwe kwa kawaida kuwa wa ukavu, baadhi ya maeneo nchini yanatarajiwa kupata mvua za nje ya msimu kutokana na mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa.
Maeneo hayo ni pamoja na Kanda ya Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara, pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Pia,TMA imeonya kuwa hali ya baridi kali pamoja na uwepo wa vumbi inaweza kuongeza hatari ya magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji, ikiwemo mafua, homa ya mapafu na matatizo ya macho, sambamba na magonjwa yanayoweza kuathiri mifugo katika maeneo mbalimbali ya wafugaji.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imezitaka jamii, wakulima, wafugaji, wavuvi pamoja na wadau wa sekta nyingine kuchukua tahadhari stahiki na kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa pamoja na tahadhari zinazotolewa mara kwa mara na TMA ili kuongeza usalama wa wananchi na ufanisi wa shughuli za kiuchumi.
Tags
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Msimu wa Kipupwe
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania



