NA DIRAMAKINI
SERIKALI imeeleza kuwa imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini baada ya kukamata tani nyingi za dawa hizo, kufanikisha hukumu katika mashauri mbalimbali ya jinai na kuimarisha huduma za tiba kwa waathirika wa uraibu.
Mafanikio hayo yamebainishwa leo Mei 29, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2025 baada ya kuiwasilisha rasmi bungeni jijini Dodoma.
Profesa Kabudi amesema,uwasilishaji wa taarifa hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 66 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015 kinachoielekeza Serikali kuandaa na kuwasilisha taarifa hiyo kila mwaka mbele ya Bunge.
Amesema,lengo la taarifa hiyo ni kuonesha uwajibikaji wa Serikali kwa wananchi kupitia Bunge pamoja na kutoa tathmini ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti dawa za kulevya nchini.
Aidha,amesema taarifa hiyo pia inalenga kutoa fursa kwa Bunge kuishauri Serikali kuhusu mbinu bora zaidi za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya ambalo limeendelea kuwa changamoto katika jamii.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bangi iliendelea kuwa dawa ya kulevya iliyokamatwa kwa kiwango kikubwa zaidi mwaka 2025 ambapo jumla ya tani 1,017.26 zilikamatwa nchini.
Hata hivyo, Waziri Kabudi amesema kiwango hicho kilipungua kwa asilimia 55.97 ikilinganishwa na mwaka 2024 kutokana na operesheni kubwa za uteketezaji wa mashamba ya bangi zilizofanyika mwaka uliopita pamoja na kuimarishwa kwa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya kilimo hicho.
Katika hatua nyingine, Serikali ilikamata tani 26.36 za mirungi, kiwango kilichoonesha ongezeko la asilimia 42.88 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Amesema,ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa operesheni za ufuatiliaji hususan katika maeneo ya mipaka na njia zinazotumiwa kusafirisha dawa hizo.
Kwa upande wa dawa za kulevya za viwandani, Serikali ilikamata kilogramu 907.18 za methamphetamine, kilogramu 672.23 za heroin, kilogramu 4.89 za cocaine pamoja na gramu 178 za MDMA na gramu 7.82 za MDA.
Profesa Kabudi amesema,kwa mara ya kwanza mwaka 2025 Serikali ilifanikiwa kukamata tani 29.52 za dawa mpya aina ya Kratom inayotokana na mmea ujulikanao kama Mitrogyna speciosa.
Amesema,dawa hiyo iliingizwa nchini ikidaiwa kuwa ni mbolea, lakini uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na mamlaka husika ulibaini kuwa ilikuwa ni dawa ya kulevya.
“Mafanikio haya yametokana na kazi kubwa iliyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika kudhibiti mitandao na njia za usafirishaji wa dawa hizo kupitia nchi kavu,anga na majini,"amesema Waziri Kabudi.
Katika jitihada za kudhibiti uchepushwaji wa kemikali bashirifu na dawa tiba zenye asili ya kulevya, amesema Serikali iliimarisha ukaguzi katika vituo vya forodha,kampuni za usafirishaji pamoja na vyombo vya usafiri.
Kupitia operesheni hizo, jumla ya tani 31.76 na lita 183.500 za kemikali bashirifu zilikamatwa pamoja na kilogramu 2.36 na mililita 160 za dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,mwaka 2025 jumla ya mashauri 1,124 yanayohusiana na dawa za kulevya yalifunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini.
Aidha, mashauri 1,373 yalitolewa hukumu ambapo Jamhuri ilishinda mashauri 1,058.
Katika hatua nyingine, mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.3 zilizohusishwa na makosa ya dawa za kulevya zilitaifishwa na Serikali.
Sambamba na operesheni za kudhibiti biashara ya dawa za kulevya, Serikali iliendelea kutoa huduma za tiba na utengamao kwa watu wenye uraibu wa dawa hizo.
Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mwaka 2025 jumla ya watu 85,425 walipata huduma za tiba kupitia vitengo vya afya ya akili katika hospitali za rufaa za mikoa na kanda, kliniki za MAT pamoja na nyumba za upataji nafuu nchini.
Amesema,Serikali pia iliendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya kupitia kampeni mbalimbali za uelimishaji katika jamii, taasisi za elimu na vyombo vya habari.
Profesa Kabudi amesema,mafanikio yaliyopatikana yametokana na dhamira thabiti ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema,Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, vyombo vya ulinzi na usalama, wataalamu wa afya na wananchi kwa ushirikiano wao uliowezesha mafanikio hayo kupatikana.
Waziri Kabudi amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini viashiria vya biashara au matumizi ya dawa za kulevya ili kusaidia kuifanya Tanzania kuwa salama na huru dhidi ya tatizo hilo.
“Ushirikiano wa wananchi ni silaha muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwani mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi za pamoja kati ya Serikali, taasisi binafsi, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla,”amesema Profesa Kabudi.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Kataa Dawa za Kulevya na Timiza Ndoto Zako
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)






