KIGOMA-Mtendaji wa Kijiji cha Kigadye wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma, Elias Kazili Bakimbaga (54) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kasulu akikabiliwa na mashtaka ya kuomba na kupokea rushwa.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani Mei 25, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, Mhe. S.A. Mchalo, katika shauri la jinai namba CC.11343/2026 la Jamhuri dhidi ya Elias Kazili Bakimbaga.Kwa mujibu wa upande wa mashtaka uliowakilishwa na Mwendesha Mashtaka kutoka TAKUKURU, Bw.Davis Junior, mtuhumiwa anakabiliwa na kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na 15(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) Sura ya 329 Marejeo ya mwaka 2023.
Ilidaiwa mahakamani kuwa Machi 22, 2026, Elias Kazili Bakimbaga alimuomba Bi. Helena Juma kiasi cha Shilingi 150,000 ili aweze kumwachia huru mume wake, Mashilimu Kinasa, aliyekuwa ameshikiliwa katika ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho kwa tuhuma za kuingia na kulima katika shamba la mtu mwingine bila ridhaa ya mmiliki.
Aidha, upande wa mashtaka ulidai kuwa Machi 23, 2026, mtuhumiwa alipokea kiasi cha Shilingi 130,000 kutoka kwa Bi. Helena Juma kama sehemu ya makubaliano hayo ili kumwachia huru Mashilimu Kinasa.
Mahakama imeelezwa kuwa, fedha hizo zilikuwa sehemu ya mtego wa rushwa uliokuwa umeandaliwa na maafisa wa TAKUKURU Wilaya ya Kasulu, ambapo mtuhumiwa alikamatwa mara baada ya kupokea fedha hizo.
Baada ya kusomewa mashtaka yake, mshitakiwa alikana kutenda makosa hayo.
Hata hivyo, mahakama ilimwachia kwa dhamana baada ya kutimiza masharti yaliyowekwa na mahakama hiyo.
Shauri hilo limeahirishwa hadi Juni 1, 2026 ambapo litatajwa tena kwa ajili ya hatua za awali za usikilizaji wa kesi hiyo.