Serikali yawasihi vijana kuepuka kushiriki migogoro ya Kimataifa

DODOMA-Serikali imeendelea kuwasihi vijana nchini kujiepusha na ushawishi wa kujiingiza katika migogoro ya kimataifa, ikiwemo vita vinavyoendelea katika baadhi ya mataifa duniani na kusisitiza umuhimu wa kutumia fursa halali za ajira na shughuli za kiuchumi zinazopatikana ndani na nje ya nchi kwa njia salama na zinazotambulika kisheria.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb), alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Jesca John Magufuli, aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuwajengea vijana uhawishi na uelewa kuhusu athari za kushiriki katika migogoro ya kimataifa.

Akijibu swali hilo, Dkt. Maghembe amesema migogoro ya kimataifa imekuwa na madhara makubwa kiuchumi, kijamii na kiusalama duniani, huku vijana wengi, hususan kutoka bara la Afrika, wakiwa miongoni mwa waathirika wakuu kutokana na kushawishiwa kujiunga na majeshi au makundi katika nchi zenye migogoro kwa matumaini ya kupata kipato.

Ameeleza kuwa hatua hiyo ni hatari kubwa kwani inaweza kuhatarisha maisha ya vijana kupitia vifo, ulemavu wa kudumu pamoja na kuwaingiza katika matatizo ya kisheria yanayokiuka sheria za nchi na sheria za kimataifa.
Amesema kuwa,kutokana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya uraia na programu za uhamasishaji kwa vijana kupitia sera, kampeni na miradi mbalimbali inayolenga kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa yao binafsi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Aidha, Serikali imeendelea kufungua fursa salama za ajira nje ya nchi kupitia ushirikiano wa kimataifa.

"Katika mwaka huu wa fedha, Serikali imefanikisha upatikanaji wa nafasi 1,500 za ajira kwa madereva nchini Qatar pamoja na nafasi 300 za wauguzi nchini Saudi Arabia, hatua inayolenga kutoa njia mbadala kwa vijana kujikwamua kiuchumi kwa njia rasmi na salama,” alisema Mhe. Maghembe.

Ameongeza kuwa, Serikali imeendelea kutekeleza programu mbalimbali za uwezeshaji vijana, ikiwemo kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo pamoja na programu za kisekta zinazoongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji, ubunifu na maendeleo ya uchumi wa taifa.
Dkt. Maghembe amesema juhudi hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa salama, wazalendo na wanashiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi badala ya kushawishika kuingia katika migogoro ya kivita inayayoweza kuhatarisha maisha yao na mustakabali wa taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here