NA DIRAMAKINI
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imemtia hatiani Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba,Bw.Alex Mutashobya Byenobi baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia manufaa isivyo halali kiasi cha Shilingi milioni 16.55 za Kitanzania zilizokuwa sehemu ya fedha za matumizi ya halmashauri kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Hukumu hiyo imetolewa leo Mei 13, 2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Janeth Massesa katika shauri la rushwa namba 10399/2026.
Mahakama ilielezwa kuwa,Bw. Byenobi alijipatia fedha hizo isivyo stahili kutoka kwenye bajeti ya matumizi ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za matumizi ya fedha za umma.
Baada ya kutiwa hatiani, mahakama ilimtaka mshtakiwa kulipa faini ya Shilingi 500,000 au kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela. Aidha,mshtakiwa amelipa faini hiyo na hivyo kuepuka kifungo.
Sambamba na adhabu hiyo, mahakama pia ilitoa amri kwa mshtakiwa kurejesha kiasi cha Shilingi 16,550,000 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Mei 13,2026.
Shauri hilo liliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. William Fussi pamoja na Bw.Daudi Jacob.
