NA DIRAMAKINI
KLABU ya Simba SC imetangaza rasmi maandalizi yake kuelekea mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi, Young Africans (Yanga), utakaopigwa Mei 3, 2026 katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na vyombo vya habari, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa, uamuzi wa kuutumia uwanja huo umetokana na maboresho yanayoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambao kwa kawaida hutumika kama uwanja wa nyumbani wa klabu hiyo.
Ameeleza kuwa,licha ya ukubwa na ubora wa Uwanja wa Mkapa, Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo umeonekana kuwa chaguo sahihi kwa sasa kutokana na ubora wa eneo lake la kuchezea.
Aidha, amesisitiza kuwa uamuzi huo haujalenga kumkwamisha mpinzani wao, bali umefanyika kwa kuzingatia mazingira yaliyopo.
Kuhusu umuhimu wa mchezo huo, Ahmed Ally amebainisha kuwa ni mechi yenye uzito mkubwa katika mbio za ubingwa wa msimu huu.
Ameeleza kuwa,matokeo ya mchezo huo yanaweza kuamua hatma ya taji la Ligi Kuu, akisisitiza kuwa ni lazima kwa Simba kushinda ili kuendelea kubaki katika ushindani wa karibu wa alama.
“Ni mechi ambayo kwa kiasi kikubwa itaamua mwelekeo wa ubingwa. Ushindi ni lazima ili kupunguza tofauti ya alama na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa taji,”amesema.
Katika taarifa yake, amethibitisha kuwa wachezaji waliokuwa majeruhi, akiwemo Oura, Kibabage na Kagoma, wamepona na wako tayari kushiriki mchezo huo muhimu. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaombea afya njema ili waweze kutoa mchango wao ipasavyo.
Kwa upande wa maandalizi, Ahmed Ally amesema kuwa, timu imehitimisha maadhimisho ya ushindi wa Kombe la Muungano na sasa imeelekeza nguvu zake zote katika mchezo wa Mei 3.
Ameongeza kuwa,ushindi katika mechi hiyo ndio utakaokamilisha furaha ya mashabiki, badala ya kufurahia mafanikio ya muda mfupi.
Ameitaja Yanga kuwa mpinzani mwenye uwezo mkubwa, akionya kuwa hawatakubali kupoteza kirahisi, hasa baada ya kukutana mara kadhaa katika kipindi kifupi.
Amebainisha kuwa,hali hiyo inaifanya mechi hiyo kuwa ngumu zaidi na yenye ushindani wa hali ya juu.
Akizungumzia malengo ya msimu, Ahmed Ally amesema Simba imelenga kurejesha heshima yake kwa kuhakikisha inashinda mataji muhimu. Ameeleza kuwa,klabu hiyo ipo tayari kupigania mafanikio katika mashindano yote inayoshiriki, ikiwemo Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho.
Kuhusu takwimu za mikutano ya timu hizo msimu huu, amebainisha kuwa tayari wamekutana mara tatu, ambapo Simba imeshinda mara mbili huku Yanga ikishinda mara moja. Aidha, aligusia mchezo mmoja uliokuwa na utata wa maamuzi ya waamuzi, akieleza kuwa taarifa ya Bodi ya Ligi ilithibitisha kuwepo kwa bao halali ambalo halikutambuliwa.
Katika hatua nyingine, klabu hiyo imetangaza viingilio vya mchezo huo, vikilenga kuwapa nafasi mashabiki wengi kuhudhuria. Viingilio vya mzunguko ni shilingi 15,000, VIP B shilingi 30,000 na VIP A shilingi 50,000.
Ahmed Ally amehimiza mashabiki kununua tiketi mapema kutokana na idadi ndogo ya nafasi za uwanja huo unaotarajiwa kuchukua takribani watazamaji 10,000.
Aidha, ameonya kuhusu uwepo wa watu wanaojaribu kununua tiketi kwa wingi (vishoka), akisema kuwa klabu imechukua hatua kwa kushirikiana na wadau husika ili kudhibiti hali hiyo.
Amehitimisha kwa kuwataka mashabiki watakaokosa tiketi kufuatilia mchezo huo kupitia matangazo ya moja kwa moja badala ya kufika uwanjani bila tiketi, akisisitiza kuwa usalama katika eneo la uwanja huo unaosimamiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) utazingatiwa kikamilifu.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku kila upande ukiwania ushindi utakaoweza kuamua hatma ya ubingwa wa msimu wa 2025/2026.
