NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala imesema imefanikiwa kufuatilia matumizi ya zaidi ya Shilingi bilioni 52 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka 2026.
Akitoa taarifa kwa umma, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ilala, Moza Kasubi amesema, taasisi hiyo imeendelea kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma pamoja na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotengwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU Ilala ilifanikiwa kusaidia kuendelea kwa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Polisi Bonyokwa wenye thamani ya Shilingi 406,645,405 baada ya kuwezesha mkandarasi kampuni ya Nyakire Investment Limited kulipwa deni la Shilingi 181,949,153.40 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi zilizokuwa tayari zimekamilika.
Imeelezwa kuwa, kabla ya hatua hiyo, mkandarasi alikuwa amesimamisha kazi kutokana na kucheleweshwa kwa malipo hayo.
Aidha, TAKUKURU Ilala imesema imefanikiwa kufuatilia utekelezaji wa miradi mingine sita yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 51.6 ambapo maboresho mbalimbali yalifanyika baada ya kubainika kwa mapungufu katika baadhi ya kazi zilizokuwa zinatekelezwa.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Kitega Uchumi Kariakoo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wenye thamani ya Shilingi bilioni 36.7, ujenzi wa barabara ya Lindi kwa kiwango cha lami wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.8 pamoja na mradi wa kisima cha maji Mchikichini wenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 164.
Miradi mingine iliyofuatiliwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 7.7, Shule ya Sekondari Kitunda Relini yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 4.2 pamoja na mradi wa kikundi cha vijana cha Fighters cha Segerea kilichopatiwa mkopo wa Shilingi milioni 40 kwa ajili ya shughuli za usafirishaji wa abiria kwa bodaboda.
Katika eneo la elimu kwa umma, TAKUKURU Ilala imesema imefanikiwa kutoa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa wananchi zaidi ya 19,320 kupitia semina, vipindi vya redio na televisheni pamoja na maonesho mbalimbali.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa klabu 33 za wapinga rushwa ziliimarishwa kupitia mafunzo kuhusu madhara ya rushwa huku semina 28 zikitolewa kwa watumishi wa umma kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu uadilifu na uwajibikaji.
Katika upande wa uchunguzi na mashitaka, TAKUKURU Ilala imesema imefanikiwa kuokoa kiasi cha Shilingi milioni 57.5 kupitia kesi ya uhujumu uchumi namba 2458/2024 iliyohusisha ubadhirifu wa fedha za Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, washtakiwa wanne katika kesi hiyo walihusika na ubadhirifu wa Shilingi milioni 115 ambapo sehemu ya fedha hizo tayari imerejeshwa katika akaunti ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania, huku kiasi kilichobaki kikitarajiwa kulipwa kwa awamu nyingine.
Aidha, TAKUKURU Ilala imeeleza kuwa katika kipindi hicho ilipokea jumla ya malalamiko 27, ambapo 26 yalihusu tuhuma za rushwa na uchunguzi wake unaendelea huku lalamiko moja likibainika kutohusiana na vitendo vya rushwa.
Mashauri mawili ya rushwa pia yamehitimishwa mahakamani ambapo Jamhuri ilishinda kesi zote, huku mashauri mengine manane yakiendelea kusikilizwa.
Kwa upande wa mipango ya Aprili hadi Juni 2026, TAKUKURU Ilala imesema itaendelea kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa uadilifu na uzalendo.
Taasisi hiyo imewataka wananchi kuendelea kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo unakuwa na tija kwa jamii pamoja na kuimarisha utawala bora nchini.
