TAKUKURU Kilimanjaro yaokoa na kurejesha shilingi milioni 16.1 za Serikali

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro imefanikiwa kusaidia kupatikana na kuokolewa kwa zaidi ya Shilingi milioni 16.1 za mapato ya Serikali pamoja na fedha za miradi ya maendeleo katika kipindi cha Januari hadi Machi,mwaka 2026.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro, Musa O.Chaulo amesema, mafanikio hayo yametokana na ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma,ukusanyaji wa mapato ya Serikali pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri mbalimbali za mkoa huo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TAKUKURU Wilaya ya Hai ilibaini kuwa,mtumishi mmoja wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi alikuwa amelipwa mishahara yenye jumla ya Shilingi milioni 11.4 kuanzia Agosti 2022 hadi Juni 2023 bila kuwapo katika kituo chake cha kazi cha Hospitali ya Marangu.

Badala yake, mtumishi huyo alikuwa akifanya kazi katika Chuo cha Uuguzi Machame kinachomilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini.

Aidha,baada ya uchunguzi huo, TAKUKURU ilimtaka mtumishi huyo kurejesha fedha zote alizolipwa pasipo kustahili, ambapo Machi 3, 2026 alirejesha kiasi hicho chote kupitia akaunti ya NMB PCCB Hai. Aidha, hatua nyingine za kisheria zinaendelea kuchukuliwa dhidi yake.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Kituo Maalumu Holili kilifanikiwa kusimamisha mkataba usio rasmi kati ya Kijiji cha Uparo na kampuni ya Million Engineering & General Supply Limited, hatua iliyosaidia kuokoa Shilingi milioni 2.5 za mapato ya kijiji hicho kilichopo Kata ya Kirua Vunjo.

Uchunguzi uliofanywa na TAKUKURU ulibaini kuwa,makubaliano hayo yalikiuka sheria, taratibu na miongozo ya ukusanyaji wa ushuru wa madini ya ujenzi.

Awali, mwekezaji huyo alitakiwa kulipa Shilingi milioni 2 kwa safari 300 za malori badala ya kiwango halali cha Shilingi 15,000 kwa kila safari, sawa na Shilingi milioni 4.5 kwa safari hizo zote.

Katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Wilaya ya Siha iliokoa mifuko 63 ya saruji ambayo ilielekezwa kutumika katika ukarabati wa darasa moja na ofisi moja katika Shule ya Msingi Olkolili baada ya kubaini kuwepo kwa ununuzi wa ziada wa saruji katika mradi wa ujenzi wa madarasa na vyoo. Uchunguzi ulionesha kuwa mifuko 105 ilinunuliwa badala ya mifuko 42 iliyohitajika.

Sambamba na hilo, TAKUKURU Siha ilisaidia fundi aliyekuwa akitekeleza mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Sabuko kulipwa Shilingi milioni 2.2 za fedha ya matazamio (retention money) ambazo alikuwa hajalipwa licha ya muda wa matazamio wa mradi kukamilika.

Kwa ujumla, TAKUKURU Mkoa wa Kilimanjaro imesema imetoa ushauri wa marekebisho ya mapungufu mbalimbali yaliyobainika katika matumizi ya zaidi ya Shilingi bilioni 15.2 zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 46 ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na uvuvi.

Katika kipindi hicho pia, taasisi hiyo ilieleza kuwa imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia semina 57, mikutano ya hadhara 35, uimarishaji wa klabu 132 za wapinga rushwa, maonesho matano, vipindi vitatu vya redio pamoja na utoaji wa habari na taarifa mbalimbali za utendaji kazi.

Kwa upande wa uchunguzi na mashtaka, TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 147, ambapo 80 yalihusu vitendo vya rushwa huku 67 yasikihusu rushwa.

Aidha, kesi nane ziliendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali za Mkoa wa Kilimanjaro, kesi mpya sita zilifunguliwa na kesi tatu zilishindwa kwa mafanikio ya upande wa mashtaka.

TAKUKURU imesema katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2026 itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa elimu kwa wananchi, kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma pamoja na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Wananchi wametakiwa kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya bure 113.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here