NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imefanikisha kurejeshwa na kuwezesha malipo ya jumla ya Shilingi milioni 58.2 kwa mamlaka mbalimbali za Serikali pamoja na watumishi wa umma kupitia shughuli zake za kuzuia rushwa katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2026.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mara, Mohamed A. Shariff amesema,fedha hizo zilipatikana baada ya uchambuzi wa mifumo mbalimbali ya usimamizi wa mapato, matumizi ya fedha za umma na utekelezaji wa mikataba katika halmashauri na taasisi za umma.
Katika hatua hiyo, TAKUKURU imefanikisha ukusanyaji wa Shilingi milioni 14.6 kutoka katika Vyombo saba vya Huduma za Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) vya Halmashauri ya Wilaya ya Musoma.
Fedha hizo zilikuwa ni sehemu ya madeni ya ankara za maji yaliyokuwa hayajakusanywa kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Uchambuzi wa TAKUKURU ulionesha kuwepo kwa udhaifu katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato, hali iliyosababisha madeni kufikia zaidi ya Shilingi milioni 84.
Baada ya mapendekezo ya TAKUKURU kufanyiwa kazi, CBWSOs hizo zilifanikiwa kukusanya asilimia 17.4 ya madeni hayo sawa na Shilingi milioni 14.6.
Aidha, TAKUKURU imewezesha malipo ya Shilingi milioni 12.6 kwa kijiji cha Seka wilayani Musoma ikiwa ni fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini ya MMG Gold Ltd.
Imeelezwa kuwa,fedha hizo zilikuwa zikipokelewa na Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kinyume na makubaliano ya mkataba wa CSR uliotaka fedha hizo kupelekwa moja kwa moja kijijini.
Kupitia uchambuzi wa mfumo wa usimamizi wa mikataba ya CSR uliofanywa na TAKUKURU, halmashauri hiyo ilielekezwa kulipa fedha hizo kwa Kijiji cha Seka kwa matumizi ya shughuli za maendeleo na kiutawala katika eneo hilo.
Katika Wilaya ya Rorya, TAKUKURU imefanikisha malipo ya Shilingi milioni 9.6 kwa Kijiji cha Nyanjage ikiwa ni mapato ya mrahaba wa viroba vya mchanga wa dhahabu kutoka mgodi wa Nyanjage.
Uchunguzi wa mfumo wa usimamizi wa mapato ya mgodi huo ulibaini kuwa,sehemu ya fedha hizo zilikuwa zimehodhiwa na kutowasilishwa kwa serikali ya kijiji kama ilivyotakiwa.
Baada ya ushauri na maelekezo ya TAKUKURU, fedha hizo zilikusanywa na kuwekwa kwenye akaunti ya kijiji huku kiasi kidogo kikitolewa kwa ajili ya posho za usimamizi na ukaguzi wa uchimbaji.
Vilevile, TAKUKURU Mkoa wa Mara imefanikisha ulipaji wa Shilingi milioni 10 kwa Wizara ya Mifugo kutoka kwa wamiliki watano wa vyombo vya uvuvi waliokuwa wamekamatwa kwa kosa la uvuvi haramu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa,wamiliki hao walicheleweshewa kutolewa kwa namba za malipo (Control Number), jambo lililokuwa na viashiria vya rushwa.
Baada ya TAKUKURU kuingilia kati, namba hizo zilitolewa na wahusika kulipa faini hiyo serikalini.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Butiama, walimu 118 wa shule za msingi na sekondari wamelipwa jumla ya Shilingi milioni 10.09 baada ya kubainika kuwa walikuwa wamepunjiwa fedha za nauli za likizo kwa mwaka 2024/2025.
TAKUKURU ilibaini kuwa,baadhi ya maafisa wa Idara ya Elimu walikata sehemu ya fedha za walimu hao na kuzitumia kulipa posho za watumishi waliohusika na mchakato wa malipo.
Kutokana na mapendekezo ya TAKUKURU, baadhi ya viongozi na watumishi wa halmashauri hiyo walirejesha fedha walizolipwa huku kiasi kingine kikitolewa kutoka katika bajeti ya matumizi ya kawaida ya idara ya elimu ili kukamilisha malipo ya walimu hao.
Kwa upande wa ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Mara imefuatilia miradi 38 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 13.3 katika sekta za afya, elimu, maji, ujenzi na utawala.
Katika ukaguzi huo, mapungufu mbalimbali yalibainika ikiwemo matumizi ya vifaa visivyo na ubora, ujenzi usiozingatia michoro sanifu pamoja na wizi wa vifaa vya ujenzi.
TAKUKURU imesema ushauri ulitolewa na hatua za marekebisho zilichukuliwa katika maeneo husika.
Pia,katika kipindi hicho, wananchi 54,231 walifikishwa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kupitia semina 54, mikutano ya hadhara 17, vipindi vya redio sita pamoja na uanzishaji na uimarishaji wa klabu 97 za kupinga rushwa.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, jumla ya malalamiko 88 yalipokelewa katika robo hiyo ambapo asilimia 63.6 yalihusu vitendo vya rushwa huku asilimia 36.4 hayakuhusisha rushwa.
Aidha, Jamhuri ilipata ushindi katika kesi tatu za rushwa huku kesi nane zikiendelea mahakamani.
TAKUKURU Mkoa wa Mara imesema,katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2026 itaendelea kuimarisha uchunguzi wa malalamiko ya rushwa pamoja na kuongeza ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma katika miradi ya maendeleo.
Pia imetoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa kupitia simu ya bure namba 113 au kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu nao.
