NA DIRAMAKINI
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuibua na kuzuia upotevu wa mapato katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.
Ni baada ya kufuatilia mfumo wa ukusanyaji ushuru wa huduma kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, ambapo zaidi ya Shilingi bilioni 1.6 zimekusanywa kutokana na hatua za kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Ezekia Sinkala kupitia taarifa kwa umma ameeleza kuwa,taasisi hiyo ilibaini baadhi ya wafanyabiashara wakifuta stakabadhi za mauzo zilizokuwa tayari zimefanyika, jambo lililosababisha kupungua kwa kiwango cha mauzo kinachooneshwa na hivyo kuathiri makusanyo ya ushuru wa huduma.
Ameeleza kuwa,uchunguzi huo pia ulibaini baadhi ya wafanyabiashara hususan wa maduka ya vifaa vya ujenzi, maduka ya jumla pamoja na wauzaji wa bidhaa za viwandani kufanya biashara bila kutoa risiti za mashine za EFD, huku wengine wakihamisha bei za bidhaa kutoka kampuni mama kwenda matawi yao kwa lengo la kupunguza kiwango cha mauzo kinachotambulika rasmi.
Kwa mujibu wa TAKUKURU, ushirikiano kati ya taasisi hiyo na uongozi wa Manispaa ya Kibaha umewezesha kuongezeka kwa mapato katika robo tatu mfululizo.
Katika robo ya kwanza, makusanyo yalifikia Shilingi bilioni 1.52, robo ya pili yakafikia Shilingi bilioni 1.80, huku robo ya tatu ikipelekea kukusanywa kwa Shilingi bilioni 1.61. Jumla ya makusanyo katika vipindi hivyo imefikia Shilingi bilioni 4.93.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Wilaya ya Kibiti imefanikiwa kuokoa mifuko 30 ya saruji yenye thamani ya Shilingi 570,000 iliyokuwa imetolewa kinyume cha utaratibu katika mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamisati.
Ukaguzi uliofanywa ulibaini kuwa,saruji hiyo ilitolewa stoo bila kuombwa wala kukabidhiwa rasmi kwa fundi anayehusika na ujenzi.
Baada ya ukaguzi huo, wahusika waliagizwa kurejesha saruji hiyo ili kuhakikisha mradi unaendelea kwa ubora unaotakiwa huku hatua nyingine za kiuchunguzi zikiendelea kuchukuliwa.
Aidha, TAKUKURU Pwani imesema imeendelea kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na barabara.
Katika kipindi hicho, miradi 55 yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10.1 ilifuatiliwa kwa lengo la kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuondoa mianya ya ubadhirifu.
Katika eneo la uchambuzi wa mifumo, taasisi hiyo imefanya chambuzi 14 pamoja na warsha tatu kuhusu utoaji wa huduma za afya kwa makundi maalum kama watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wanaoishi na virusi vya UKIMWI katika wilaya zote za Mkoa wa Pwani.
Baadhi ya maazimio yaliyotolewa ni pamoja na kutoa mafunzo endelevu kwa wahudumu wa afya kuhusu huduma kwa watu wenye mahitaji maalum, kuboresha miundombinu ya vyoo na kuongeza faragha kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya UKIMWI.
Kwa upande wa elimu kwa umma, TAKUKURU Pwani imesema imewafikia wananchi zaidi ya 41,963 kupitia mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, maonesho na semina mbalimbali zilizolenga kuongeza uelewa kuhusu madhara ya rushwa na wajibu wa wananchi katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Katika kipindi hicho pia, TAKUKURU ilipokea taarifa 71 kutoka kwa wananchi, ambapo taarifa 53 zilihusu vitendo vya rushwa na zinaendelea kufanyiwa kazi katika hatua mbalimbali za uchunguzi.
Kesi saba zilikamilika mahakamani, huku Jamhuri ikishinda kesi tano, kesi tatu mpya zikifunguliwa na kesi 14 zikiendelea kusikilizwa.
Kwa upande wa mipango ya Aprili hadi Juni 2026, TAKUKURU Pwani imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia semina, mikutano ya hadhara na vipindi vya redio sambamba na kuimarisha shughuli za uchunguzi, uzuiaji na uendeshaji wa mashauri ya rushwa mahakamani.
Taasisi hiyo imewataka wananchi wa Mkoa wa Pwani kuendelea kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kwa kutoa taarifa sahihi kupitia namba za simu 113 bila malipo pamoja na kufika moja kwa moja katika ofisi za TAKUKURU.
.jpeg)