TAKUKURU Rukwa yashinda rufaa ya kesi ya Uhujumu Uchumi dhidi ya aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kalaela wilayani Kalambo

NA DIRAMAKINI

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Rukwa imeendelea kuonesha mafanikio katika vita dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi baada ya kushinda rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kalaela Wilaya ya Kalambo,Bw. Leonard Noah Kayula.
Kayula alikuwa akipinga hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela kwa makosa ya rushwa, ubadhirifu na kuisababishia Serikali hasara.

Mafanikio hayo yameelezwa na Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Rukwa, Thomas Msuta katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka 2026.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga ilitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Bw.Leonard Noah Kayula dhidi ya Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi namba 12944/2025.

Bw. Kayula ambaye alikuwa Mtendaji wa Kijiji cha Kalaela katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo awali alihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kila kosa pamoja na kuamriwa kurejesha kiasi cha Shilingi milioni 8.4 alizobainika kuzifanyia ubadhirifu wakati wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo.

Shauri hilo la rufaa lilisikilizwa mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Abubakari Mrisha ambapo mshtakiwa alikuwa anakata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa dhidi yake katika Mahakama ya Wilaya ya Kalambo.

Kwa mujibu wa TAKUKURU, mshtakiwa alipatikana na hatia katika makosa matatu ambayo ni matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA) Sura ya 329, ufujaji na ubadhirifu kinyume na Kifungu cha 28 cha sheria hiyo pamoja na kosa la kuisababishia Serikali hasara kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi Sura ya 200.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa,makosa hayo yalitendwa katika kipindi cha kuanzia Julai 1, 2017 hadi Novemba 15, 2021 wakati mshtakiwa akiwa mtumishi wa umma.

Baada ya Mahakama ya Wilaya ya Kalambo kutoa hukumu dhidi yake Aprili 29, 2025, mshtakiwa alikata rufaa katika Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Sumbawanga, lakini Machi 27, 2026 Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa yake na kuthibitisha hukumu iliyotolewa awali.

Kutokana na uamuzi huo, mshtakiwa anatakiwa kutekeleza adhabu ya kifungo pamoja na kurejesha fedha zote alizofanyia ubadhirifu.

Ufuatiliaji wa Miradi ya Bilioni 2.7

Mbali na ushindi huo wa kesi, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa pia imeendelea kufuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija iliyokusudiwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya miradi 16 yenye thamani ya Shilingi bilioni 2.7 imefanyiwa ufuatiliaji katika kipindi hicho.

Katika ukaguzi huo, TAKUKURU ilibaini changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa vifaa vya ujenzi katika maeneo ya miradi, ushirikishwaji mdogo wa wananchi pamoja na mapungufu katika mchakato wa zabuni.

Kutokana na hali hiyo, taasisi hiyo ilitoa mapendekezo mbalimbali likiwemo kuimarishwa kwa tathmini za zabuni ili kupata wazabuni wenye uwezo, kuhakikisha sheria na kanuni za utekelezaji wa miradi zinafuatwa pamoja na kuongeza ushirikishwaji wa wananchi tangu mwanzo hadi mwisho wa utekelezaji wa miradi.

Aidha,katika juhudi za kuzuia vitendo vya rushwa, TAKUKURU Rukwa imeendelea kutoa elimu kwa umma kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio pamoja na kuanzisha na kuimarisha klabu za wapinga rushwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa,wananchi wapatao 4,887 walifikishiwa elimu ya mapambano dhidi ya rushwa katika kipindi hicho.

Elimu hiyo imesaidia kuongeza mwitikio wa wananchi katika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa mamlaka husika.
Malalamiko 93 Yapokelewa

Katika upande wa uchunguzi, TAKUKURU Mkoa wa Rukwa imepokea jumla ya malalamiko 93 katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.

Kati ya malalamiko hayo, 53 yalihusu rushwa sawa na asilimia 57 huku malalamiko 40 ambayo ni asilimia 43 hayakuhusu rushwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa,malalamiko yasiyohusu rushwa yalitolewa ushauri kwa wahusika, huku yale yaliyohusu rushwa yakifunguliwa majalada ya uchunguzi na hatua za kisheria kuendelea.

Aidha, kesi nne ziliendelea kusikilizwa mahakamani katika kipindi hicho ambapo kesi moja ilitolewa hukumu na Jamhuri ilishinda.
Wananchi Watakiwa Kutoa Taarifa

TAKUKURU Mkoa wa Rukwa imewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kujiepusha na vitendo hivyo.

“Rushwa haliipi, hivyo wananchi waendelee kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya simu 113 bila malipo au kwa kuwasiliana na ofisi ya TAKUKURU Mkoa,” alisema Bw. Msuta.

Aidha, taasisi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea na mikakati yake ya kuelimisha umma, kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi.

Kaulimbiu ya TAKUKURU inayosema “Kuzuia Rushwa ni Jukumu Lako na Langu; Tutimize Wajibu Wetu” imeendelea kusisitizwa kama msingi wa mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here