Vijana soka lenu

NA LWAGA MWAMBANDE

TIMU ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Vijana ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys imeandika historia baada ya kutinga hatua ya fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) kufuatia ushindi wa penalti dhidi ya Misri U-17 katika mchezo wa nusu fainali.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa ulimalizika kwa sare tasa ndani ya dakika 90 za kawaida kabla ya Serengeti Boys kufanikiwa kuibuka na ushindi wa penalti 4-3 na kutinga rasmi hatua ya mwisho ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Katika mchezo huo, vijana wa Tanzania walionesha nidhamu kubwa ya mchezo, uimara wa safu ya ulinzi pamoja na utulivu wa kisaikolojia wakati wa upigaji wa penalti, hali iliyowapa ushindi muhimu dhidi ya wenyeji hao wa Afrika Kaskazini.

Ushindi huo umeendelea kuamsha furaha kubwa kwa mashabiki wa soka nchini huku ukiiweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la Afrika kwa vijana kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.

Kutokana na matokeo hayo, Serengeti Boys sasa itakutana na Senegal U-17 katika mchezo wa fainali baada ya Senegal kuiondoa Morocco U-17 katika mchezo mwingine wa nusu fainali.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anabainisha kuwa,mafanikio ya Serengeti Boys yanaashiria kukua kwa kiwango cha soka la vijana nchini Tanzania, huku akisifu uwekezaji unaoendelea kufanywa katika kukuza vipaji vya vijana kupitia mashindano ya ndani na programu za maendeleo ya soka.Endelea;

1. Nyie vijana wetu, mmetuheshimisha,
Ushindi mwema kwetu, mmetufurahisha,
Fainali ni yetu, mlivyotuvumisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

2. Kuwatoa vigogo, sana mmetukosha,
Mmepanua wigo, wa kujitambulisha,
Kwenye soko ni zogo, watu mwagombanisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

3. Algeria chali, mlivyowadondosha,
Hata na Misri chali, mlivyowalowesha,
Sasa ni Senegali, mwaweza kuwafisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

4. Hongera wachezaji, jinsi mmetukosha,
Makocha ni mtaji, mlipowafikisha,
Tumeona vipaji, mmejitambulisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

5. Heri twawatakia, fainali yatosha,
Muweze kufikia, kombe kujibebesha,
Tuzidi furahia, mlipotufikisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

6. Na kombe la dunia, mmeshatufikisha,
Huko twasubiria, mwende tuwakilisha,
Itajwe Tanzania, mzidi tuvumisha,
Vijana soka lenu, ni la kimataifa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here