NA GODFREY NNKO
KILA mwaka ifikapo Mei 20, Dunia huadhimisha Siku ya Vipimo Duniani kwa lengo la kuhamasisha umuhimu wa vipimo sahihi katika maisha ya kila siku,biashara,afya, teknolojia, viwanda na maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Maadhimisho ya mwaka 2026 yanabebwa na kauli mbiu isemayo, “Vipimo hujenga imani katika uundaji wa sera.”
Kauli hii inaonesha kwa uzito namna mifumo sahihi ya vipimo ilivyo msingi wa maamuzi bora ya kitaifa, upangaji wa maendeleo na ustawi wa wananchi.
Nchini Tanzania, jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo linatekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), taasisi inayohakikisha mizani, pampu za mafuta, mita za umeme, vipimo vya bidhaa na vifaa mbalimbali vya kupimia vinatumika kwa usahihi ili kulinda maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Ikumbukwe kuwa, katika mazingira ya sasa ya ukuaji wa uchumi,biashara na maendeleo ya teknolojia,ushirikiano wa karibu kati ya wananchi,sekta binafsi,taasisi za umma na Wakala wa Vipimo ni jambo lisiloepukika.
Ushirikiano huo si kwa ajili ya kulinda haki za watumiaji pekee, bali pia kuimarisha uadilifu wa biashara, kuongeza mapato ya Serikali na kujenga mazingira yenye ushindani wa haki katika uchumi.
Katika maisha ya kila siku, wananchi hutegemea vipimo katika huduma mbalimbali ikiwemo ununuzi wa bidhaa sokoni, mafuta ya magari, huduma za maji, umeme, gesi na bidhaa za viwandani. Endapo vipimo vitakuwa si sahihi, mlaji ndiye anayekuwa mwathirika wa kwanza.
Mfano rahisi ni katika vituo vya mafuta.Ikiwa pampu ya mafuta haitoi kiwango halisi kinacholipiwa, mwananchi hupata hasara bila kujua.
Vivyo hivyo katika masoko ya nafaka, nyama, sukari au bidhaa nyingine zinazouzwa kwa uzito, mizani isiyo sahihi huweza kusababisha udanganyifu mkubwa kwa walaji na wafanyabiashara waaminifu.
Hivyo basi, wananchi wanapaswa kushirikiana na WMA kwa kutoa taarifa wanapobaini viashiria vya udanganyifu katika vipimo.
Ushirikiano huo husaidia kudhibiti vitendo vya ubadhirifu, kulinda haki za mlaji na kujenga mazingira bora ya biashara.
Mathalani,wadau wa sekta binafsi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha vipimo vinazingatiwa. Wamiliki wa viwanda,vituo vya mafuta, maduka,maabara,migodi na biashara nyingine wanapaswa kuhakikisha vifaa vyao vya kupimia vinakaguliwa na kuthibitishwa mara kwa mara na WMA.
Kuzingatia vipimo sahihi huongeza imani kwa wateja na hujenga sifa nzuri ya biashara. Aidha, biashara inayofuata sheria za vipimo huwa na uwezo mkubwa wa kushindana katika soko la ndani na kimataifa kutokana na kuaminika kwa bidhaa na huduma zake.
Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaendelea kukuza uchumi wa viwanda, uwekezaji na biashara ya kimataifa, suala la viwango na vipimo sahihi limekuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.
Bidhaa zinazokidhi vipimo sahihi hupata nafasi kubwa ya kukubalika katika masoko ya kimataifa na kuongeza mapato ya Taifa.
Sekta ya afya ni miongoni mwa maeneo yanayotegemea vipimo kwa kiwango kikubwa. Vipimo vya dawa,vifaa tiba,mashine za maabara na huduma za kitabibu vinahitaji usahihi wa hali ya juu ili kulinda maisha ya watu.
Dosari ndogo katika vipimo vya dawa au vifaa tiba inaweza kusababisha madhara makubwa kwa wagonjwa. Hali kadhalika katika sekta ya ujenzi, vipimo visivyo sahihi vinaweza kusababisha majengo yasiyo salama na kuhatarisha maisha ya wananchi.
Kwa msingi huo, taasisi zote zinazotumia vifaa vya kupimia zinapaswa kushirikiana na WMA kuhakikisha vifaa hivyo vinathibitishwa mara kwa mara kwa mujibu wa sheria na viwango vilivyowekwa.
Mbali na kulinda walaji, vipimo sahihi vina mchango mkubwa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Katika sekta kama mafuta,madini, gesi,umeme na maji, matumizi ya vipimo sahihi husaidia kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki kutokana na shughuli za uzalishaji na biashara.
Endapo vipimo vitakuwa haviko sahihi, Taifa linaweza kupoteza mapato makubwa kupitia mianya ya udanganyifu au ukwepaji wa kodi.
Ndiyo maana usimamizi madhubuti wa vipimo ni sehemu muhimu ya ujenzi wa uchumi imara na wenye uwazi.
Kauli mbiu ya mwaka huu inayosema, “Vipimo hujenga imani katika uundaji wa sera,” inaonesha kuwa takwimu na maamuzi mengi ya Serikali hutegemea mifumo sahihi ya vipimo.
Serikali inapopanga sera za afya, biashara, kilimo,viwanda,mazingira au nishati, hutegemea takwimu zinazokusanywa kupitia mifumo ya vipimo.
Iwapo vipimo vitakuwa visivyo sahihi,hata sera zinazotungwa zinaweza kushindwa kuleta matokeo yaliyokusudiwa.
Hivyo, uwepo wa vipimo sahihi husaidia viongozi na watunga sera kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.
Pamoja na jitihada zinazofanywa na WMA, mafanikio makubwa yanategemea ushirikiano wa wananchi wenyewe. Wananchi wanapaswa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu haki zao wanapotumia huduma zinazohusisha vipimo.
Ni muhimu kwa wananchi kuhakikisha mizani, pampu za mafuta au vifaa vingine vinavyotumika katika huduma vina alama za ukaguzi kutoka WMA.
Pale wanapobaini udanganyifu au ukiukwaji wa sheria za vipimo, wanapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
Kwa kufanya hivyo, jamii itasaidia kujenga mfumo wa biashara wenye haki, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha uchumi wa Taifa.
Hitimisho
Katika dunia ya sasa inayotegemea sayansi, teknolojia na biashara za kisasa, vipimo sahihi si jambo la hiari bali ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya Taifa lolote.
Ushirikiano kati ya wananchi, wadau wa sekta mbalimbali na Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ni nguzo muhimu ya kuhakikisha haki, uwazi na maendeleo vinapatikana katika nyanja zote za maisha.
Maadhimisho ya Siku ya Vipimo Duniani mwaka 2026 yanapaswa kuwa chachu ya kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa vipimo sahihi na wajibu wa kila mmoja katika kulinda mfumo huo.
Kwa pamoja, Taifa linaweza kujenga uchumi wenye kuaminika, biashara zenye haki na huduma bora kwa wananchi kupitia utamaduni wa kuthamini vipimo sahihi.
