MWANZA-Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, amewahimiza wafanyabiashara jijini Mwanza kuwekeza kwenye mifumo ya kisasa ya usalama kwa kufunga kamera za CCTV katika maeneo yao ya biashara.
Akizungumza leo Mei 14, 2026, wakati akitoa elimu ya usalama kwa wafanyabiashara wa Soko la Mirongo, wilaya ya Nyamagana, SSP Sodoka amesisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo ni msaada mkubwa katika kuwatambua na kuwatia mbaroni wahalifu kwa haraka pindi matukio ya uvunjaji yanapotokea.
Alibainisha kuwa kamera hizo huondoa utata wa kile kilichotokea kwani hurekodi muda halisi, wahusika, na mazingira yote ya tukio.
Sambamba na hayo, SSP Sodoka amewataka baadhi ya wafanyabiashara wanaoajiri walinzi wenye umri mkubwa, kuacha mara moja kwani hawana uwezo wa kuhimili majukumu ya ulinzi usiku kucha.
Amesema kuwa wazee hao mara nyingi huishiwa nguvu na kulala wakiwa kazini, jambo ambalo hutoa mwanya kwa wahalifu kufanya uharibifu.
Badala yake, amewashauri wafanyabiashara kutumia kampuni binafsi za ulinzi zenye sifa, weledi na vijana wenye nguvu ili kuhakikisha kuwa mali zinazoachwa sokoni jioni zinapatikana zikiwa salama asubuhi inayofuata.
Kwa upande mwingine, Polisi Kata wa Mirongo, INSP Fatuma Mpinga, amewatahadharisha wafanyabiashara kuhusu mbinu mpya zinazotumiwa na wahalifu, ikiwemo kujenga mahusiano ya karibu na wafanyakazi wa madukani.
INSP Mpinga ameeleza kuwa wahalifu wengi hujifanya wateja waaminifu kwa muda mrefu mpaka wanapofanikiwa kuingia kwenye mahusiano ya kimapenzi na wafanyakazi, hatua inayowarahisishia kupata siri za biashara na taarifa za kifedha.
Amewataka wamiliki wa biashara kuwapa elimu ya mara kwa mara wafanyakazi wao ili waweze kutofautisha kati ya huduma kwa mteja na mahusiano yanayoweza kuhatarisha usalama wa biashara zao.


