DAR-Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, ametoa wito kwa vijana waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita mwaka 2026 kutoka shule zote za Tanzania Bara na Visiwani kuhudhuria Mafunzo ya JKT Kundi la Lazima (Mujibu wa Sheria) kwa mwaka 2026.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena, amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti makambini kuanzia Juni 1 hadi Juni 7, 2026.Akitoa taarifa hiyo leo Mei 28, 2026 jijini Dodoma, amesema sambamba na wito huo, JKT limewapangia vijana hao makambi mbalimbali watakayokwenda kupatiwa mafunzo.
Makambi hayo ni pamoja na Rwamkoma JKT-Mara, Msange JKT-Tabora, Ruvu JKT na Kibiti JKT-Pwani, Mpwapwa JKT na Makutupora JKT-Dodoma, Mafinga JKT-Iringa, Mlale JKT-Ruvuma, Mgambo JKT na Maramba JKT-Tanga, Makuyuni JKT na Oljoro JKT-Arusha, Bulombora JKT, Kanembwa JKT na Mtabila JKT-Kigoma, Itaka JKT-Songwe, Luwa JKT na Milundikwa JKT-Rukwa, Nachingwea JKT-Lindi pamoja na Chuo cha Uongozi JKT (CUJKT) Kimbiji kilichopo Dar es Salaam.
Aidha, wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical Disabilities) wametakiwa kuripoti katika Kambi ya Ruvu iliyopo Mlandizi mkoani Pwani kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kuwahudumia.
JKT pia limewataka vijana hao kuripoti wakiwa na vifaa muhimu vikiwemo bukta ya rangi ya dark blue yenye mpira kiunoni, T-shirt ya kijani, raba za michezo za kijani au blue, shuka mbili za blue bahari, soksi nyeusi, nguo za kuzuia baridi kwa waliopangiwa maeneo yenye baridi, track suit ya kijani au blue pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohitajika katika udahili wa kujiunga na elimu ya juu.
Vifaa vingine vilivyotajwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na nauli ya kwenda kuripoti makambini na kurudi nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, orodha kamili ya majina ya vijana waliochaguliwa, makambi waliyopangiwa, maeneo yalipo makambi hayo pamoja na vifaa vinavyotakiwa, inapatikana kupitia tovuti ya JKT.
Aidha, ili kufahamu kambi aliyopangiwa, mhusika atatakiwa kuingiza jina la shule au namba ya shule aliyohitimu kidato cha sita, ambapo mbele ya jina la shule ataona neno “waliochaguliwa” na baada ya kulichagua ataona majina ya waliochaguliwa kujiunga na mafunzo hayo pamoja na kambi, wilaya na mkoa alikopangiwa.
Ili kuona majina yote ya vijana pamoja na makambi walizopangiwa, mtumiaji atapakua faili la JKT PDF 2026 lililowekwa juu kulia katika ukurasa huo.
Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Nduku Mabele, anawakaribisha vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2026 kujiunga na wenzao katika kujengewa uzalendo, kufundishwa nidhamu, ukakamavu, umoja wa kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha pamoja na utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa.