TMA,EMEDO waja na tuzo za kipekee kwa waandishi wa habari Tanzania

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) leo Mei 28,2026 imetangaza rasmi ushirikiano wa Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu changamoto za matukio ya hali mbaya ya hewa, na utoaji wa tahadhari za mapema, na usalama kwenye maji hapa Tanzania.
Meneja Masoko na Uhusiano kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania,Bi. Monica Mutoni akizungumza katika mkutano huo.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Mbezi Garden jijini Dar Es Salaam, Bi.Mary Francis Mahemba, Afisa Uchechemuzi (Advocacy Officer) kutoka Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) amesema kuwa,vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuifikia jamii kwa taarifa sahihi zinazoweza kusaidia kuokoa maisha, kupunguza athari za majanga yanayohusiana na hali ya hewa,pamoja na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu usalama majini.
“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi
na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga. Kupitia tuzo hizi tunatambua mchango wao katika kujenga jamii salama na inayotambua hatari za kuzama maji,” alisema Bi. Mary Francis Mahemba.

Tuzo hizi zinalenga kuhamasisha utayarishaji wa habari zenye ubora kuhusu:

1. Matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii;

2. Tahadhari za mapema za hali ya hewa;

3. Usalama wa vyombo vya usafiri na usafirishaji kwenye maji

4. Uzuiaji wa ajali na vifo vitokanavyo na kuzama maji;

5. Ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayohusiana na hali ya hewa.

Kwa muktadha huu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la EMEDO wameandaa Tuzo zitakazowahusisha waandishi wa Habari.

Tuzo hizo zitahusisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii na
majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.

Waandishi wanaalikwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia tarehe
1/08/2025 mpaka tarehe 30/08/2026.

Kazi zote zitumwe kwenye barua pepe hizi mbili media@meteo.go.tz / mediahaliyahewa@gmail.com
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Bi. Monica Mutoni, Meneja Masoko na Uhusiano, alisisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa na mifumo ya tahadhari za mapema katika kuokoa maisha ya wananchi, hususan wale wanaotegemea shughuli za maji kama vile uvuvi na usafiri wa majini.

Bi Monica alisema, TMA imeendelea kuhakikisha mchango wa wanahabari utambulika kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa kuongeza thamani za Tuzo za Wanahabari wa Masuala ya Hali ya Hewa nchini.

Ushirikiano katika tuzo hizi ni sehemu ya juhudi za kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari katika kuimarisha uelewa,
usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here