SINGIDA-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba leo Jumapili Mei 31, 2026 amekagua ujenzi wa Barabara ya Noranga (Doroto)–Itigi (Mlongojii) yenye urefu wa kilomita 25 inayojengwa katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa gharama ya shilingi bilioni 29.6.

Akipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Miradi wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko, Dkt. Mwigulu alielezwa kuwa hadi Mei 30, 2026 mradi huo umefikia asilimia 83.25 ya utekelezaji ambapo kilomita 20.2 zimekamilika kwa kiwango cha lami huku kilomita 4.8 zilizobaki zikiwa zimejengwa hadi tabaka la juu la msingi na zinatarajiwa kukamilika Juni 30, 2026.
Mhandisi Nnko alisema kipande hicho ni sehemu ya Barabara ya Mbeya–Chunya–Makongolosi–Rungwa–Itigi–Mkiwa yenye urefu wa kilomita 524 inayounganisha mikoa ya Mbeya, Singida na Tabora na ambayo inatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa watu, bidhaa na mazao katika ukanda huo.
Amesema,mradi huo unagharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na unatekelezwa na Kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) kutoka China kwa gharama ya shilingi 29.6 bila VAT.
Aidha, alisema kazi za ujenzi zilianza Septemba 16, 2022 na zinatarajiwa kukamilika Agosti 7, 2026 baada ya mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji kwa mujibu wa mkataba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi Mei 30, 2026 mkandarasi alikuwa amelipwa shilingi bilioni 12.9 na alikuwa anadai shilingi bilioni 3.84. Aidha, Mhandisi Mshauri alikuwa amelipwa shilingi bilioni 1.49 na anadai shilingi milioni 586.6.
Pia, wananchi 578 ambao mali zao ziliathiriwa na mradi huo wamelipwa fidia ya jumla ya shilingi milioni 721.4 kwa mujibu wa sheria.
Katika utekelezaji wake, mradi huo umezalisha ajira 305 ambapo ajira 278 sawa na asilimia 91 zimetolewa kwa wazawa na ajira 27 sawa na asilimia 9 zimetolewa kwa wageni.








