DODOMA-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema imesikitishwa na kile ilichodai kuwa ni upotoshaji wa taarifa pamoja na usambazaji wa matamshi yasiyo sahihi kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii kufuatia Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara imeeleza kuwa,taarifa hizo zimekuwa zikisambazwa baada ya hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kuwasilishwa Bungeni Mei 26,2026.Wizara imefafanua kuwa,baadhi ya maudhui yanayosambazwa mitandaoni yamepotosha kwa makusudi ujumbe halisi wa hotuba hiyo kwa lengo la kuleta mkanganyiko kwa wananchi pamoja na kuathiri taswira ya Tanzania na misingi yake ya diplomasia, uhuru na mshikamano wa kitaifa.
Kutokana na hali hiyo, Wizara imesisitiza kuwa itaendelea kutoa ufafanuzi rasmi kupitia vyombo vya habari pamoja na majukwaa mbalimbali ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye muktadha kamili kuhusu masuala yaliyojadiliwa katika hotuba hiyo ya bajeti.
Aidha, Wizara imepongeza namna ambavyo vyombo mbalimbali vya habari nchini vimeendesha mjadala wa kitaifa kuhusu hotuba hiyo, huku ikieleza kuwa mjadala huo umeonesha mshikamano wa kitaifa pamoja na kuunga mkono michango ya wabunge waliotetea umuhimu wa kulinda uhuru, hadhi na utaifa wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mjadala huo unaonekana kuwa ishara ya ukomavu wa diplomasia ya Tanzania, mfumo wa demokrasia pamoja na uzalendo wa wananchi katika kusimamia maslahi ya taifa, hasa katika kipindi ambacho kumekuwa na mijadala ya kimataifa kuhusu misimamo ya baadhi ya mataifa ya nje katika masuala ya ndani ya nchi nyingine.
Serikali kupitia Wizara hiyo imeeleza kuwa, itaendelea kusimamia kwa uthabiti misingi ya uhuru wa taifa, kutokuingiliwa katika mambo ya ndani ya nchi pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia unaozingatia usawa, heshima na maslahi ya pande zote kwa mujibu wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.
Sambamba na hilo, Wizara imetoa wito kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii, wadau wa habari pamoja na wananchi kwa ujumla kutumia uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia maadili, sheria za nchi, weledi wa taaluma pamoja na wajibu wa kulinda amani, mshikamano na heshima ya taifa.