Ahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa tuhuma za mauaji Mbeya

MBEYA-Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya imemhukumu kunyongwa hadi kufa, Barnaba Daud Mtewele mkazi wa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kumtia hatiani kwa mauaji ya Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbugani, Herieth Lupembe (37), Ivon Tatizo mwanafunzi wa kidato cha pili wa Isenyela Sekondari na kumjeruhi mtoto wake Daud Barnaba Mtewele mwenye umri wa miaka saba Machi 30,2024.
Awali katika kesi hiyo ya jinai namba 6799/2025 ilikuwa itolewe hukumu Mei 29,2026 lakini iliahirishwa kutokana na Jaji kupata udhuru hivyo kuiahirisha hadi Juni 3,2026 ambapo Jamhuri imewakilishwa na Wakili Augustino Magesa na mshitakiwa Barnaba Mtewele amewakilishwa na Wakili wa kujitegemea Joyce Kasebwa.

Akitoa hukumu iliyodumu kwa saa mbili kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 11:30 jioni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mheshimiwa Joackim Charles Tiganga amemtia hatiani Barnaba Daud Mtewele kwa makosa matatu.

Kati ya hayo, makosa mawili ni ya mauaji ya Mwalimu Herieth Lupembe na Ivon Tatizo pia kujeruhi Daud Barnaba Mtewele ambaye alilazwa Hospitali ya Wilaya ya Chunya,Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Benjamin Mkapa.

Akisoma hukumu Jaji Tiganga amesema, upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi nane pamoja vielelezo mbalimbali na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi wanne na kielelezo kimoja.

Ilielezwa mahakamani kuwa, Barnaba Mtewele alizaa na Mwalimu Herieth Lupembe mtoto Daud Barnaba aliyetoa ushahidi wake mbaye aliieleza mahakama kuwa, mara kadhaa baba yake alikuwa akija mara kwa mara na kula pamoja na wakati mwingine kuingia chumbani na siku ya tukio anachokumbuka baba yake alimpiga mama yake na dada yake kwa sururu kisha naye alipigwa na sururu.

Aidha, shahidi baada ya kupigwa na sururu alipoteza fahamu na kuvuja damu nyingi ambapo baada ya siku kadhaa alipata fahamu ndipo alipoeleza kuwa muhusika wa matukio yote ni baba yake mzazi licha ya kuulizwa na Waakili wa utetezi bado ushahidi haukutingisha.

Shahidi mwingine ni ndugu wa Herieth aliyeiambia mahakama kuwa, Daud akiwa hospitali alimwambia kuwa baba yake ndiye aliyempiga na sururu mama yake,dada yake na yeye.

Katika ushahidi mwingine ni daktari aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu Herieth na Ivon ambaye aliimbia mahakama kuwa vifo vimesababishwa na mvujo wa damu nyingi.

Pia Askari wa Upelelezi Wilaya ya Chunya alitoa ushahidi ambapo alisema, alipokea taarifa kutoka kwa balozi baada ya kumtafuta kwa simu na kwenda kwake milango yote ilikuwa imefungwa kwa ndani ndipo walipovunja walikuta miili ina majeraha na damu ikiwa imetapakaa na Polisi walipofika walikuta eneo la tukio kuna sururu na miili miwili ilithibitishwa kuwa ni ya Herieth, Ivon na mtoto Daud ambaye alikuwa amepoteza fahamu.

Ushahidi mwingine uliotolewa ni pamoja Daktari aliyemtibu Daud Barnaba aliyedai kuwa Daud alijeruhiwa katika fuvu la kichwa na kuvuja damu nyiingi hali iliyosababisha kupoteza fahamu.

Mhemiwa Jaji Joackim Tiganga amesema, kifungu cha 117 na 118(iiii)(a) sura ya 6 iliyofanyiwa marejeo 2023 inautaka upande wa mashitaka kuthibitisha pasipo shaka kwa kuona au ushahidi wa kimazingira pia kuzingatia kifungu cha 211(i)((ii),211(a) na 380(i) sura yya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2003 ambayo inamtia hatiani mtu yeyote mwenye nia ya kutenda kosa,kupanga hata kama kiitendo hicho hakijafikia mwisho.

Upande wa utetezi mshitakiwa alileta mashahidi wanne na kielelezo kimoja ambacho ni cheti cha ubatizo kwani mshitakiwa alidai siku ya tukio hakwenda nyumbani kwa Herieth badala yake alikuwa ibadani Kanisa la Anglikana Chunya alikosimamia ubatizo na yeye kurejea nyumbani ingawa ushahidi wake haukuthibitishwa na mkewe kuwa siku hiyo alirejea nyumbani au la.

Pia ushahidi wa Katekista Mapunda,Joyce, Kayombo hauthibitishi kuwa baada ya ibada mshitakiwa alikuwa wapi licha ya kuwasilisha cheti cha ubatizo bado hakioneshi kusajiliwa katika kitabu cha kanisa.

Baada ya kusikiliza pande zote mbili Wakili wa Serikali, Augustino Magesa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kwa mujibu wa sheria ambapo wakili wa utetezi kuiomba mahakama kuona namna ya kutoa adhabu kwa mtuhumiwa ni kosa lake la kwanza.

Jaji alihitimisha shauri hilo kwa kumhukumu Barnaba Mtewele kunyongwa hadi kufa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua Herieth Lupembe na Ivon Tatizo pia kifungo cha miaka kumi kwa kumjeruhi, Daud Barnaba.

Rufaa iko wazi kwa upande ambao haujaridhishwa na uamuzi uliotolewa.Nje ya Mahakama Wakili wa Serikali  Augustino Magesa na Geofrey Kibasa wameridhishwa na hukumu iliyotolewa na Jaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here