NA DIRAMAKINI
MHANDISI Mwajuma Waziri, ni mama mzazi wa watoto watano anayebeba taji la “Malkia wa nguvu katika Sekta ya Maji”. Amejenga jina sio tu kama mama shupavu wa familia bali pia kiongozi mwenye weledi mkubwa. Kwa uchache alizaliwa na kukulia mkoani Tabora alipoanzia safari ya kuisaka elimu na kujikita katika taaluma yake.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri akionyesha tuzo aliyonyakua ya “Malikia wa Nguvu” hivi karibuni jijini Dodoma.Hivi sasa, kwa utendaji kazi katika kuwatumikia wananchi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji. Ni matokeo baada ya kuanza safari ya kuwatumikia wananchi katika Utumishi wa Umma mapema mwaka 2013.
Ni safari iliyoanza kitambo kirefu kwa maisha ya mwanadamu na bado inaendelea sababu haijafika katika ukingo katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kabisa.
Alizaliwa Septemba 1984 akiwa mtoto wa tatu katika familia ya marehemu Mzee Juma Waziri Kambangwa na Bi. Tabu Ramadhani Kagisa.
Tangu mwezi Machi 2024 hadi leo Mhandisi Mwajuma anatumika kuwahudumia Watanzania katika nafasi ya juu katika Utumishi wa Umma kwa kuongoza kazi zote za Sekta ya Maji hapa nchini.
Awali, amewahi kuhudumu nafasi ya Naibu Katibu Mkuu mwaka 2023, pia nafasi ya Mkurugenzi Msaidizi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kati ya mwaka 2020 na 2023.
Ni mmbobezi katika Sekta ya Maji kwa taaluma na uzoefu wa kazi akiwa Mhandisi rasmi na mwenye usajili wa bodi inayohusika na utaalam huo hapa Tanzania. Mhandisi Mwajuma ana Shahada ya Uzamili (MSc) na Shahada ya Kwanza (BSc) katika Uhandisi wa Ujenzi na Rasilimali za Maji aliyotunukiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Ujuzi wake umejikita katika usanifu wa mifumo ya maji, usimamizi wa miradi, taratibu za zabuni, pamoja na matumizi ya programu za kitaalamu katika uhandisi ikiwemo program ya Kompyuta inayotumika kuchambua mifumo ya usambazaji wa maji (EPANET), program ya kuchora na kubuni kwa kutumia Kompyuta (AutoCAD), na program ya Kompyuta ya utekelezaji wa kazi za Kihandisi ikiwamo ujenzi wa bomba za usambazaji majisafi na maji taka (Civil 3D).
Eneo alilobahatika kufungua pazia katika Utumishi wa Umma ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, kusini mwa Tanzania. Ni hapo ndipo alianza kuiweka taaluma yake kwa vitendo bila kujali jinsia au kuchagua kazi za “site”, ikiaminika kwa wengi katika jamii ni wanaume pekee wanaoweza kazi ngumu za ujenzi katika miradi ya maji.
Ndani ya jamii wapo ambao hapo mwanzo ilikuwa ngumu kuamini kazi za Sekta ya Maji zinaweza kutekelezwa na jinsi ya kiume pekee, kwamba kazi ni znito na inahitaji nguvu pia kukaa au kuishi mbali na makazi. Mhandisi Mwajuma katika kazi ya Uhandisi alionesha kuwa hayo yalikuwa mawazo yasiyokuwa na uhalisia kwa kufanya kazi bila kutetereka.
Utendaji na uzoefu katika kazi kwa weledi umeweza kumuibua kuwa kinara na kupokea tuzo mbalimbali hadi leo hii.
Tuzo ya siku za usoni aliyonyakua miongoni mwa wengi ikiwa ni ile ya “Malkia wa nguvu katika Utumishi wa Umma 2026” ikiwa ni kielelezo cha kutambua kazi kubwa anayofanya kama kiongozi akiwa kielelezo tosha kwa kina mama wengine.
Kuhusu usanifu na usimamizi wa miradi ya maji kazi hii ameonyesha kuimudu kwa vitendo na uwezo mkubwa. Baadhi ya miradi ameshiriki kwa kazi usiku na mchana ikiwamo mradi mkubwa wa usambazaji maji wa miji 28, mradi wa maji wa bwawa la Farkwa, mradi wa Same-Mwanga-Korogwe pamoja na mradi wa ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi wa Simiyu.
Hiyo ni michache kati ya miradi ya maji mingi, mikubwa na midogo, ambapo baadhi ya miradi hiyo wananchi tayari wananufaika na huduma ya majisafi na salama.
Kwa ushiriki huu katika ujenzi wa miradi ya maji, ameonyesha uwezo mkubwa wa kuratibu wadau, kusimamia michakato ya kitaalamu, na kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio kwa matokeo hususan kwa miradi iliyoleta sintofahamu awali ‘chechefu’ ikiwemo mradi wa maji wa Same - Mwanga – Korogwe, mradi ambao ni fupa ambalo hatimaye limetafunwa na Serikali ya Awamu ya Sita. Kumbukumbu, nyaraka mbalimbali na simulizi za viongozi mbalimbali inaonyesha ni mradi uliokaa muda mrefu tangu miaka ya 70.
‘’Katika Taifa hili kuna maeneo nikifika naona mchango wangu kama Mhandisi. Hii kazi sio rahisi inahitaji dhamira ya dhati pia kushirikiana na wataalamu wengine katika kufanikisha. Hii ni moja ya fahari kubwa katika kutimiza majukumu ya kutoa huduma kwa wananchi” Mhandisi Mwajuma anasema akiongea na mwandishi ofisini kwake.
Anasema kuwa uongozi hauchagui jinsia bali uwezo katika kuitambua na kuishirikisha anuwai ya jamii kwa kuangalia mahitaji kutimiza mpango wa Serikali uliokusudiwa.
‘’Sisi wanawake tunaweza kuwa katika nafasi mbalimbali ili kufanikisha lengo lililokusudiwa, kuanzia nyumbani, na tusiwe watu wakurudi nyuma kwa kuhofia mitazamo hasi kwa kuhisi kwamba nafasi na fursa zinazokuwepo ni ngumu. Tuwajenge watoto wa kike kwa mtazamo chanya waelewe kuwa fursa zenye kuleta maendeleo zinapojitokeza wawe na uthubutu wa kuzikimbilia bila kurudi nyuma," Mhandisi Mwajuma anasema.
‘’Taaluma ya Uhandisi wa maji kwa sisi wanawake bado tupo wachache, nikirejea mfano wa darasa nililosoma mimi tulikuwa hatuzidi wanawake 10 na wanaume walikuwa wengi, lakini hii haibadilishi haiba yoyote unaweza kuwa Mhandisi na ukaendelea kuwa na haiba ya kike, hivyo nahimiza sana kwa watoto wa kike katika jamii kuanzia ngazi ya sekondari kupenda masomo ya Sayansi na kuwatia moyo kuwa wanaweza kufanya vizuri pengine kuliko wanaume,’’ Mhandisi Mwajuma anasema.
Kwa maisha katika jamii ni nikama jua linapo chomoza kwa Mhandisi Mwajuma. Ni taswira ya kioo inayotazamwa na wengi ili kuleta mabadiliko yenye kuleta maendeleo endelevu kuanzia Sekta ya Maji hadi maeneo mengine katika taifa kwa kuwapa morali watoto wa Tanzania kuweka mkazo katika masomo na fursa zinazojitokeza.
Kuhusu kazi anasema suala la utendaji huwezi kupata matokeo bila kuwa na mazingira bora ya kazi kwa watumishi ambapo Wizara ya Maji imejipanga kwa kuweka mazingira bora pahala pa kazi ikiwemo vitendea kazi, na majengo.
Anaongeza kuwa anaona fahari kubwa kuwa sehemu ya mafanikio ya Sekta ya Maji ikiwemo kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi kwa asilimia 93.5 kwa maeneo ya mijini na asilimia 85.3 kwa maeneo ya vijijini.
Hatua hii Mhandisi Mwajuma anasema ni sawa na kugawa tabasamu kwa kila Mtanzania kwa sababu maji ni rasilimali muhimu ambayo haina mbadala sio kama soda, ukikosa Pepsi basi utakunywa soda ingine jamii ya Coke na kwa uhalisia bila maji hakuna maisha ya mwanadamu na viumbe hai wengine pamoja na mazingira.
Mhandisi Mwajuma amewahi kuwa mzungumzaji katika mikutano mikubwa ya kimataifa ikiwamo Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika Dubai mwaka 2023, pamoja na Jukwaa la 10 la Dunia la Maji lililofanyika katika jiji la Bali, nchini Indonesia mwaka 2024. Kupitia majukwaa haya, aliweza kuchangia mijadala kuhusu usalama wa maji, ustahimilivu wa tabianchi, na uwekezaji katika Sekta ya Maji.
‘’Kwa sasa nikiwa Katibu Mkuu hamasa kubwa ninayoitoa ni kuendelea na utekelezaji wa mkakati wa usimamizi wa utekelezaji wa Mkakati wa Gridi ya Maji ya Taifa na kukamilisha kufikisha huduma ya maji katika vijiji 1,575 ambavyo bado havijapata huduma ya rasmi ya majisafi nchini, pia nahimiza watendaji na wataalamu wote kufanyakazi kwa juhudi kubwa ili kukamilisha mkakati huo kwa kuwashirikisha wananchi katika kila hatua’’ Mhandisi Mwajuma anasema.
Ni kwa uwazi na hakuna kificho kuwa tunaweza kumtazama Mhandisi Mwajuma kama historia inavyo mulika mashujaa wengine wanawake wanaoleta mchango mkubwa katika taifa hili linaloongozwa na Rais wa kwanza Mwanamke katika ukanda wa Afrika Mashariki, Rais Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan.
Hivyo basi, Mhandisi Mwajuma Waziri ni moja ya mfano wa uongozi bora na wenye weledi katika Sekta ya Maji nchini. Kupitia uzoefu, ubunifu, taaluma na kujitolea kwake katika Utumishi wa Umma, ameweka mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji, utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Tanzania.
Katika safari yake ya elimu ya awali Mhandisi Mwajuma alihudhuria elimu ya msingi katika shule mbalimbali huko Tabora zikiwemo shule ya msingi Isevya mwaka 1991-1993 na Shule ya Msingi Ipuli mwaka 1993-1997.
Baada ya hapo alijiunga na shule ya sekondari ya Kazima mwaka 1997-1999 kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne, na masomo ya elimu ya juu katika shule ya sekondari Mkwawa ambapo alifanikiwa kumaliza vizuri kidato cha sita.
Tunasema “Thamani ya Almasi ipo daima”, maji ni chachu ya kukuza Sekta nyingine katika jamii, na umuhimu wa Mhandisi Mwajuma katika fani yake upo, kwa kuwashirikisha wananchi na kuwapa mahaba ya huduma ya maji mjini na vijijini kwa kiwango bora kabisa.