Bodi ya Ligi yatoa adhabu kali kwa wachezaji, klabu na mashabiki wa Ligi Kuu na Championship

Magata afungiwa michezo mitano, TRA United yapigwa faini ya Shilingi milioni 16, mashabiki wa Simba na Yanga wafungiwa viwanjani

NA DIRAMAKINI

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali dhidi ya wachezaji, klabu na mashabiki kufuatia ukiukwaji wa kanuni uliojitokeza katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Championship ya NBC, huku ikisisitiza umuhimu wa kuzingatia taratibu za mashindano na nidhamu katika soka la Tanzania.
Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Juni 8, 2026 baada ya kupitia taarifa za waamuzi, makamishna wa mechi pamoja na ushahidi wa matukio yaliyojitokeza viwanjani.

Katika hatua inayodhihirisha msimamo mkali wa TPLB katika kulinda uadilifu wa mchezo, mchezaji wa Mtibwa Sugar, Magata Fredrick amefungiwa michezo mitano na kutozwa faini ya Shilingi 500,000 kwa kosa la kurudi uwanjani na kushiriki mchezo baada ya kufanyiwa mabadiliko.

Taarifa ya TPLB imeeleza kuwa,baada ya kutolewa nje ya mchezo dhidi ya TRA United, Magata alirejea uwanjani wakati timu yake ikiwa katika hali ya kujihami dhidi ya shambulio la wapinzani, hatua iliyofanya Mtibwa Sugar kuwa na wachezaji 12 ndani ya uwanja kwa muda mfupi.

Baada ya shambulio hilo kumalizika, mchezaji huyo aliondoka uwanjani huku akijaribu kujificha nyuma ya wachezaji wenzake ili asionekane na waamuzi.

TPLB imeeleza kuwa,kitendo hicho ni ukiukwaji wa Kanuni ya 17:30 kuhusu Taratibu za Mchezo.

Kwa upande wa TRA United, klabu hiyo imejikuta ikitozwa faini ya jumla ya Shilingi milioni 16 kutokana na makosa yanayomhusisha Kocha Mkuu wake, Etienne Ndayiragije.

Katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, TRA United ilitozwa faini ya Shilingi milioni tano baada ya Ndayiragije kushindwa kuhudhuria mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika siku moja kabla ya mchezo bila kutoa taarifa rasmi, huku akiwakilishwa na kocha msaidizi kinyume cha kanuni za mashindano.

Aidha, katika mchezo dhidi ya Fountain Gate, klabu hiyo ilitozwa faini nyingine ya Shilingi milioni 11 baada ya kocha huyo kurudia kosa hilo kwa mara nyingine.

TPLB imebainisha kuwa,licha ya kupewa maelekezo na kukumbushwa juu ya wajibu wake, Ndayiragije alishindwa kuhudhuria mikutano ya waandishi wa habari katika michezo mitano mfululizo.

Katika mchezo uliowakutanisha Coastal Union na Simba SC, mchezaji wa Coastal Union, Meshack Abraham, amefungiwa michezo mitatu baada ya kukutwa na hatia ya kumfanyia rafu ya hatari mchezaji wa Simba, Anicet Oura, kitendo kilichotafsiriwa kuhatarisha usalama wa mchezaji mwenzake.

Wakati huo huo, Klabu ya Simba SC imepigwa faini ya Shilingi milioni tano kufuatia matukio yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC.

Kwa mujibu wa TPLB, mtoto mmoja wa kuokota mipira alichukua chupa za maji zilizokuwa karibu na eneo la goli la Dodoma Jiji, akamwaga maji yaliyokuwamo na baadaye kuondoka na taulo la mlinda mlango wa timu hiyo.

Taarifa imeeleza kuwa,baada ya tukio hilo, mlinda mlango wa Dodoma Jiji pamoja na mchezaji Andy Bikoko walimfuata mtoto huyo wakimtaka kurejesha taulo hilo.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa karibu na eneo hilo walianza kurusha chupa zenye vimiminika kuelekea kwa wachezaji hao.

TPLB imesema,vitendo hivyo vinakiuka misingi ya uungwana na vinaathiri taswira ya mchezo wa soka nchini.

Katika adhabu nyingine, mshabiki wa Simba, Omary Omary maarufu kwa jina la "Bomba", amefungiwa kuingia viwanjani kwa muda wa miezi 12 baada ya kufanya vurugu katika vyumba vya kubadilishia nguo vya Dodoma Jiji na kutoa tuhuma zinazohusiana na imani za kishirikina dhidi ya mmoja wa viongozi wa klabu hiyo.

Kwa upande wa Young Africans (Yanga), mashabiki wawili maarufu wa klabu hiyo, Baraka Shekimweri maarufu kama "Baraka Yanga" na Abdulrahman Saidi maarufu kama "Fumau Mshairi", wamefungiwa kuingia viwanjani kwa muda wa miezi mitatu.

Mashabiki hao walikamatwa wakikiuka utaratibu wa maeneo ya kuketi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kulazimisha kuingia katika eneo la VIP A huku wakiwa na tiketi za VIP B.

Taarifa imeeleza kuwa,walipuuzia maelekezo ya maafisa wa tiketi na kuvuka uzio unaotenganisha maeneo hayo.

Katika Ligi ya Championship ya NBC, Klabu ya Mbuni ya Arusha imetozwa faini ya Shilingi milioni moja kwa kuchelewa kuingia uwanjani katika mchezo dhidi ya TMA, hatua iliyotafsiriwa kuwa kutoheshimu ratiba rasmi ya matukio ya mechi.

Pia mchezaji wa Mbuni, Yunus Lema ametozwa faini ya Shilingi 500,000 baada ya kukwepa kushiriki zoezi la kupeana mikono na timu pinzani kabla ya mchezo kuanza licha ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

Kwa upande wa African Sports ya Tanga, klabu hiyo imepewa onyo kali baada ya kuwakilishwa na wajumbe wanne badala ya watano katika kikao cha maandalizi ya mechi dhidi ya Polisi Tanzania, jambo lililokiuka masharti ya kanuni za mashindano.

Hatua ya TPLB kutoa adhabu hizi inaonekana kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha nidhamu, uwajibikaji na uendeshaji wa kitaalamu wa ligi za soka nchini, huku wadau wa mchezo huo wakihimizwa kuzingatia kanuni na taratibu zote zilizowekwa ili kulinda hadhi na maendeleo ya soka la Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here