DODOMA-Bodi ya Wakurugenzi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye pia ni Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, leo tarehe 18 Juni 2026 imemtembelea Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), jijini Dodoma na kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Benki Kuu.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Omar amesisitiza kuwa,Benki Kuu ina nafasi muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, ukuaji wa sekta binafsi, pamoja na maendeleo jumuishi ya uchumi.
Aidha, ameipongeza Benki Kuu kwa usimamizi thabiti wa sekta ya fedha, hususan benki za biashara, hatua iliyochangia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu hadi kufikia chini ya asilimia 5.
Pamoja na pongezi hizo, alihimiza Benki Kuu kuendelea kufanya maboresho na mageuzi zaidi katika sekta ya fedha ili kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake, Gavana Tutuba alieleza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza kwa uthabiti sera ya fedha, pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei, ili kuhakikisha uwepo wa mazingira wezeshi ya ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi.


