NA DIRAMAKINI
KUFUATIA mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, Rais wa Jamhuri ya Namibia, anatarajiwa kufanya Ziara ya Kitaifa nchini Tanzania kuanzia tarehe 19 hadi 21 Juni, 2026.
Wakati wa ziara hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia atafanya mazungumzo ya pande mbili na Mheshimiwa Rais Dkt. Nandi-Ndaitwah kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika sekta
mbalimbali.
Viongozi hao wawili pia wanatarajiwa kushuhudia utiaji saini wa Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) katika sekta muhimu pamoja na kuhutubia mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.
Ziara hiyo pia ina umuhimu wa kipekee kutokana na uhusiano wa muda mrefu wa Mhe. Rais Nandi-Ndaitwah na Tanzania. Wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika ikiwemo Namibia, Tanzania ilikuwa makazi ya pili kwa wapigania uhuru na viongozi wengi wa Namibia.
Aidha, Mhe. Rais Nandi-Ndaitwah aliishi na kufanya kazi nchini Tanzania akiwa sehemu ya harakati za kupigania uhuru wa Namibia, na atatumia fursa hiyo kutembelea tena maeneo yenye umuhimu wa kihistoria kwa Namibia na yeye binafsi, ikiwemo Magomeni jijini Dar es Salaam na Makaburi ya Wapigania Uhuru wa Namibia yaliyopo Kongwa mkoani Dodoma.
Kwa sasa, nchi hizi mbili zinaendelea kushirikiana kwa karibu kupitia Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (Joint Permanent Commission of Cooperation - JPCC) pamoja na ushirikiano kupitia mashirika ya kikanda na kimataifa kama vile Umoja wa Afrika (AU),Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Mataifa (UN) na Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).
Ziara hii inaonesha dhamira ya pamoja ya Tanzania na Namibia kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuimarisha ushirikiano wa uwili, na kuongeza biashara kwa manufaa ya wananchi
wa nchi zote mbili.

